• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
Barabara Naromoru-Kieni hazipitiki

Barabara Naromoru-Kieni hazipitiki

Na SAMMY WAWERU

WAKAZI wa Wadi ya Naromoru/Kiamathaga, Kieni kaunti ya Nyeri wanaiomba serikali kuwajengea barabara kwani nyingi yazo eneo hilo hazipitiki kutokana na hali yake duni.

Wanalalamika kutaabika katika shughuli za usafiri na uchukuzi hususan msimu wa mvua.

Kulingana na baadhi ya wakazi tuliozungumza nao, wanateta wanakabiliwa na wakati mgumu kusafiri na hata kusafirisha au kubeba mizigo.

Eneo hilo ni tajika katika kilimo.

“Sisi wenyewe hata kutembea ni shida, mazao ya kilimo yanaozea shambani kwa sababu ya barabara mbovu ilhali viongozi wetu ni kueneza siasa tu,” mwenyeji wa kijiji cha Gitinga, na kilichoonekana kuathirika pakubwa aliambia Taifa Leo.

Wengi wanategemea ukuzaji wa mboga, viazimbatata, vitunguu, maharagwe na mimea mingine inayokua kwa muda wa miezi mitatu. Pia, hulima mahindi yanayochukua kipindi kifupi kuzalisha.

Barabara ya kuingia katika kijiji hicho ni ya udongo wa kufinyanga, suala ambalo linafanya mambo yazidi unga wakati wa mvua.

Wakazi walisema magari ni nadra kuingia humo wakati wa mvua, kwa hofu ya kukoma na hata kukesha.

“Wanafunzi wanasafirishwa kwa basi asubuhi na jioni wanapitia wakati mgumu. Kuna wanaokosa kuenda shuleni msimu wa mvua,” alilalamika mkazi mwingine.

Bodaboda ambazo zinasaidia kurahisisha uchukuzi pia nazo zinakwama kwenye matope kwa sababu ya hali mbaya ya barabara.

Ili kusafirisha mazao ya kilimo, wanatumia trekta ambayo pia inakwama.

Kanini Kega ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya biashara na viwanda bungeni ndiye mbunge wa Kieni.

Wadi ya Naromoru/Kiamathaga inaongozwa na MCA Martin Matu.

Mgao wa fedha

Kila mwaka serikali kuu hutengea maeneobunge yote nchini hazina ya maendeleo, CDF, ambayo pia inapaswa kuangazia miundo msingi kama barabara.

Serikali za kaunti pia zinajukumika kuwajibikia ujenzi wa barabara kupitia madiwani, MCA.

Bw Timothy Mburu, mkulima Gitinga ndiye amejitolea kukarabati mojawapo ya barabara kwa kumwaga mawe. “Kufikia sasa barabara ninayoshughulikia imenigharimu zaidi ya Sh50, 000. Ni aibu kuona viongozi wetu wametufumbia macho. Tangu tuwachague, hatujawahi kuwaona humu, wanasubiri wakati wa kuomba kura,” akalalamika Mburu.

You can share this post!

Huenda Victor Wanyama akaondoka Spurs

Hakimu katika kesi ya Waititu ajiuzulu

adminleo