Makala

DAU LA MAISHA: Anapiga vita ulanguzi wa watu na utumwa

June 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA taifa ambalo viwango vya ukosefu ajira vinaendelea kuongezeka, Wakenya wengi wamekuwa wakitafuta fursa za ajira katika mataifa ya mbali kwa matumaini ya kukwepa umaskini.

Harakati hizi kwa wengi zimewapeleka mataifa ya kigeni na hasa nchi za Mashariki ya Kati, huku wengi wakiangukia mikono ya mabosi katili na kuishia kuteswa, kujeruhiwa na hata baadhi yao kurejeshwa nyumbani wakiwa maiti.

Hii ni sababu kuu ambayo imemsukuma Mandy Gupta Vasudev kujitwika jukumu la kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu ziara hizi ambazo mara nyingi huwaingiza hatarini.

Bi Vasudev ni mwanzilishi wa ‘My Body Belongs To Me’, mradi ambao umekuwa ukihamasisha vijana hasa kutoka vitongoji duni kuhusu hatari za kusafiri kuelekea nchi za kigeni kiholela eti kwa matumaini ya kupata ajira.

Hasa mradi huu umekuwa ukihamasisha watoto na vijana kuhusu ulanguzi wa watu na utumwa, vile vile jinsi ziara hizi zinavyowaweka kwenye hatari ya kuuawa na viungo vyao vya mwili kuibiwa.

Kulingana naye, mara nyingi vijana hawa husafiri bila ufahamu tosha kuhusu waendako. “Hasa tunalenga vijana kutoka vitongoji duni kwa sababu wao ndio mara nyingi wanakabiliwa na ukosefu wa ajira. Wengi wao wana viwango duni vya elimu na ndio hunaswa na fursa hizi ghushi kuhusu kazi ughaibuni,” aeleza.

Ujumbe wao ni kwamba sio vibaya kusafiri kwenda kufanya kazi katika mataifa ya kigeni, lakini kabla ya kwenda huko, unapaswa kuwa na ufahamu na ujuzi wa kutosha utakaokuwezesha kupata ajira upesi.

Kupitia mradi huu wamekuwa wakizuru shule na makanisa katika vitongoji duni ambapo wao huandaa warsha na vikao vya majadiliano ya ana kwa ana na watoto, vile vile vijana.

“Baadaye sisi huwahimiza kuwasiliana kupitia sanaa kama vile michoro ukutani yaani ‘graffiti’ inayotoa ujumbe wa jinsi ya kuheshimu miili yao, suala linalojitokeza kupitia wimbo wetu tuliotunga… My body belongs to me, Don’t touch me. I’m Gods child, I’m born free. Respect me…Aidha, tumekuwa tukiandaa michezo ya drama mitaani, densi na mashairi,” aeleza.

Kufikia sasa wametembelea mitaa ya Kibra, Mathare, miongoni mwa mingine, na kuandaa zaidi ya warsha kumi.

Bi Vasudev alihamia humu nchini miaka mitano iliyopita kutoka Dubai. Ni akiwa hapa ambapo alipata fursa ya kufanya kazi na mashirika mbalimbali ya kimataifa.

“Nilikutana na raia mmoja wa Ujerumani ambaye alinihamasisha kuhusu masuala ya amani katika sekta ya kijamii, ustawi na jinsi ya kukabiliana na mizozo katika jamii miongoni mwa mambo mengine,” aeleza.

Uchu wake wa kutaka kujihusisha na masuala haya ulimjia baada ya kutazama habari kuhusu utumwa kwenye kituo cha habari cha kimataifa ya CNN. “Huo ulikuwa mwaka wa 2015 ambapo habari kuhusu visa vya utumwa nchini Libya hasa dhidi ya raia kutoka mataifa ya magharibi mwa Afrika zilikuwa zimechacha. Taarifa hizi zilinihuzunisha na kunishawishi niingilie kati angalao kuokoa vijana,” aeleza.

Ufahamu wa kutosha

Aliona haja ya kuhamasisha watu na hasa vijana kuhusu hatari za kuhamia mataifa ya kigeni pasipo kuwa na taarifa na ufahamu wa kutosha.

“Niliona haja ya kuhamasisha watu kuhusu hatari za kusafiri kuelekea ng’ambo bila ufahamu wa kutosha hasa kuwafahamisha vijana kwamba mipaka ya nchi yao inawalinda na pindi wanapovuka, inakuwa rahisi kwao kudhulumiwa,” aeleza.

“Aidha msukumo wangu unatokana na sababu kuwa nimesoma vitabu vingi kuhusu utumwa ambavyo vimebadilisha maisha yangu kwa jumla,” asema.

Kulingana Bi Vasudev, sharti vyombo vya habari pia vihusike vilivyo kwa kuangazia taarifa kuhusu ulanguzi wa watu, utumwa na mateso mengine. “Kinga ni bora zaidi ya tiba, hii ndio kauli mbiu muhimu ya kukabiliana na tatizo hili,” aongeza.