• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
VIWANGO BORA FIFA: Kenya nambari 105 duniani

VIWANGO BORA FIFA: Kenya nambari 105 duniani

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars ya Kenya imepanda nafasi tatu kutoka 108 hadi 105 kwenye viwango bora vya soka duniani vya FIFA vilivyotangazwa Ijumaa.

Vijana wa kocha Sebastien Migne wameimarika kutokana na ushindi wao mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya wanavisiwa wa Madagascar katika mechi yao ya kwanza ya kirafiki kabla ya Kombe la Afrika (AFCON) 2019.

Stars ilichabanga Barea ya Madagascar 1-0 jijini Paris nchini Ufaransa mnamo Juni 7 kupitia penalti ya nahodha Victor Wanyama, ambaye husakata soka yake ya malipo katika klabu ya Tottenham Hotspur nchini Uingereza.

Ushindi huu umewezesha mabingwa hawa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kubadilishana nafasi ya 108 na Madagascar na pia kuruka Libya ambayo imesalia katika nafasi ya 105 kwa tofauti ya alama.

Kwenye jedwali hili la mataifa 211 wanachama wa FIFA, Kenya ina jumla ya alama 1207 kutoka 1202 katika viwango bora vilivyopita hapo Aprili 4, 2019.

Libya imesalia na alama 1207 nayo Madagascar ina alama 1198 kutoka 1203 ilizokuwa nazo mwezi Aprili.

Senegal, ambayo Kenya itakutana nayo katika mechi za Kundi C kwenye AFCON mnamo Julai 1 jijini Cairo, imeruka juu nafasi moja hadi nambari 22 duniani.

Teranga Lions ndiyo ya kwanza barani Afrika. Inafuatiwa na Tunisia, ambayo pia imeimarika kutoka 28 hadi 25 baada ya kunufaika na Romania na Japan kuteremka chini nafasi mbili kila mmoja hadi nambari 27 na 28 mtawalia. Nigeria, Morocco, DR Congo na Ghana zimesalia katika nafasi tatu, nne, tano, sita na saba barani Afrika, lakini zimeporomoka kwenye viwango vya FIFA.

Super Eagles ya Nigeria iliyokabwa na Warriors ya Zimbabwe 0-0 mjini Asaba, imeshuka nafasi tatu hadi 45 duniani, Atlas Lions ya Morocco ambayo iliduwazwa na Scorpions ya Gambia 1-0 imeteremka nafasi mbili hadi nambari 47 duniani nayo Leopards ya DR Congo ikashuka kutoka 46 hadi 49 baada ya kulazimishiwa sare ya 0-0 dhidi ya Stallions ya Burkina Faso. DR Congo itakabana koo na Kenya katika mechi ya kirafiki mnamo Juni 15 jijini Madrid nchini Uhispania.

Black Stars ya Ghana ilishangazwa 1-0 na Brave Warriors ya Namibia na kuteremka kutoka 49 hadi nambari 50.

Mabingwa watetezi wa AFCON, Cameroon wamepaa nafasi tatu hadi nambari 51 duniani baada ya kuchapa Chipolopolo ya Zambia 2-1. Indomitable Lions pia ilinufaika na Ugiriki na Montenegro kutupwa chini nafasi tisa na mbili hadi nambari 52 na 53 mtawalia.

Misri, ambayo inashikilia rekodi ya mataji mengi ya AFCON (saba), imeteremka nafasi moja chini hadi nambari 58 duniani. Kuteremka kwake kulichangiwa na Finland kupepeta Bosnia & Herzegovina na Liechtenstein kwa mabao 2-0 kila mmoja katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Bara Ulaya (Euro) mwaka 2020.

Ivory Coast na Mali, ambazo pia zinaenda AFCON, zimeimarika kwa nafasi tatu hadi nambari 62 duniani kila mmoja. Algeria, ambayo Kenya itaanza nayo katika kampeni ya AFCON hapo Juni 23, imeruka juu kutoka 71 hadi 69 duniani.

Waalgeria walikabwa 1-1 na Burundi katika mechi ya kirafiki mnamo Juni 11. Walinufaika na Guinea kubwagwa 1-0 na Benin hapo Juni 11. Guinea inashikilia nafasi ya 71 baada ya kushuka nafasi tatu, alama moja mbele ya nambari 72 Afrika Kusini ambayo imeruka juu nafasi moja, licha ya kusalia na alama 1135.

Uganda, ambayo iko kundi moja na Misri, DR Congo na Zimbabwe kwenye AFCON, imeteremka nafasi moja hadi nambari 80 duniani. Zimbabwe imerukia nafasi ya 109 kutoka 110 duniani. Namibia imesalia katika nafasi ya 113 duniani.

Guinea-Bissau, ambayo pia iko AFCON, haijasonga kutoka nafasi ya 118, Angola imeshuka nafasi moja hadi 123, Tanzania imekwamilia nafasi ya 131 nayo Burundi, ambayo ndiyo timu inayoshikilia nafasi ya chini sana katika AFCON mwaka 2019, iko juu nafasi mbili hadi 134 duniani.

Eneo la Cecafa

Katika eneo la Cecafa, Uganda ni ya kwanza (chini nafasi moja hadi 80 duniani) ikifuatiwa na Kenya (juu nafasi tatu hadi 105 duniani), Sudan (imesalia 130 duniani), Tanzani (imekwamilia 131 dunaini), Burundi (juu nafasi mbili hadi 134 duniani), Rwanda (juu nafasi mbili hadi 136 duniani), Ethiopia (inasalia 150 duniani), Sudan Kusini (chini nafasi moja hadi 168 duniani), Djibouti (juu nafasi mbili hadi 195 duniani), Eritrea (nafasi moja juu hadi 202 duniani) na Somalia (juu nafasi moja hadi 202 duniani).

Hakuna mabadiliko katika nafasi nne za kwanza duniani ambazo zinashikiliwa na Ubelgiji, Ufaransa, Brazil na Uingereza, huku mabingwa wapya wa Ligi ya Mataifa ya Bara Ulaya Ureno wakirukia nafasi ya tano kutoka saba.

Croatia, ambayo mwanasoka bora duniani mwaka 2018 Luka Modric anachezea, iko chini nafasi moja hadi nafasi ya sita.

Inafuatiwa na Uhispania (nafasi mbili juu), Uruguay (nafasi mbili chini), Uswizi (nafasi moja chini) nayo Denmark imesalia katika nafasi ya 10.

Mabingwa wa zamani wa Kombe la Dunia Ujerumani na Argentina wameshikilia kwa pamoja nafasi ya 11, ingawa Ujerumani imepiga hatua mbili mbele.

Italia inashikilia nafasi ya 14 baada ya kuruka juu nafasi tatu nayo Uholanzi pia iko katika nafasi hiyo ikiimarika kwa nafasi mbili.

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Anapiga vita ulanguzi wa watu na utumwa

MWANAMKE MWELEDI: Sasa yuko mbioni kudumisha amani

adminleo