• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Walimu wa lugha wawika kwenye tuzo

Walimu wa lugha wawika kwenye tuzo

Na WINNIE ATIENO na MISHI GONGO

MSHINDI wa tuzo za mwalimu bora mwaka huu (TOYA) Bw Fredrick Shikuku na mwalimu mbunifu zaidi Bi Catherine Wanjiku Mune hufunza lugha katika shule za upili za St Marys Yala na Kerugoya mtawalia.

Bw Shikuku mwalimu wa somo la Kingereza na Fasihi alikuwa mwalimu wa kiume wa pekee aliyepata tuzo washindi walipotangazwa katika kongamano la 44 la walimu wakuu wa shule za upili lililofanyika mjini Mombasa.

Bi Mune aliyesomea katika shule ya msingi ya Thika na shule ya upili ya wasichana ya Muthira kabla ya kujiunga na chuo cha Kenyatta, hufunza dini ya Kikristo na Kiswahili.

“Nashukuru Mwenyezi Mungu kwa ushindi huu, kumekuwa na mikakati mingi kumuinua mtoto wa kike, serikali na jamii kwa jumla imewekeza zaidi katika kuboresha mtoto wa kike, ndiposa kati ya nafasi tatu zilizoshindaniwa nafasi mbili zimechukuliwa na wanawake,” alisema Bw Shikuku huku akitabasamu.

Mwalimu huyo alipokea kipakatalishi na hundi ya Sh100,000 miongoni mwa zawadi nyingine.

Bw Shikuku mwenye umri wa miaka 44 alisema amekuwa akifunza kwa muda wa miaka 18, na hivi sasa ni mkuu wa idara ya lugha katika Shule ya Upili ya St Marys.

“Nimekuwa nikipata msaada kutoka kwa familia yangu, mwalimu wangu mkuu, Mkurugenzi wa elimu katika kaunti yangu, walimu wenzangu na hata wanafunzi,” alisema Bw Shikuku.

Mwalimu huyo alisema kuwa hakuwa na nia ya kuwa mwalimu lakini wazazi wake walimshinikiza na hatimaye akakubali.

“Wazazi wangu walikuwa walimu bora na mimi nilipoanza masomo ya ualimu niliapa kuwa nitakuwa mwalimu bora nchini, leo hii namshukuru Mola kwa kuikamilisha ndoto yangu,” alisema.

Bw Shikuku anapanga kutumia pesa alizozawadiwa kuwanunulia sare wanakwaya katika kanisa analoshiriki.

Kiingereza

Mwalimu huyo alisomea katika Shule ya Msingi ya Tigoi na ya Upili ya Wavulana ya Nyang’ori na hatimaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta alikosomea shahada ya somo la Kingereza na Fasihi na kuhitimu mwaka wa 1998.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Othaya, Kaunti ya Nyeri, Jane Waceke, mwenye umri wa miaka 48 alipata tuzo ya mwalimu mkuu bora (POYA).

“Nimekuwa mwalimu kwa miaka 25. Nilisomea katika Shule ya Msingi ya Gitunduti, kisha kujiunga na Shule ya Upili ya Kiambu na baadaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Moi kwa shahada ya Elimu kisha nikajiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kwa shahada ya uzamili,” alisema Bi Waceke ambaye amehudumu kama mwalimu mkuu kwa miaka 12.

Bi Waceke aliwahimiza wanafunzi hususan wa kike kutia bidi katika masomo yao.

You can share this post!

Ruto ashambulia ODM kupendekeza Raila arithi Uhuru

KINAYA: Eti wazee Mlimani wamtukana Ruto kumfurahisha...

adminleo