• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Pigo jipya kwa juhudi za IEBC kuteua mrithi wa Chiloba

Pigo jipya kwa juhudi za IEBC kuteua mrithi wa Chiloba

Na WALTER MENYA

MCHAKATO wa kumtafuta Afisa Mkuu Mpya Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) umepoteza dira kwa mara nyingine baada ya kampuni iliyoteuliwa kuwachuja waliorodheshwa kukataa kazi hiyo.

Mara ya kwanza kufeli kwa mchakato huo ilikuwa Mei 20 wakati Mahakama ya Uajiri na Leba iliposimamisha uteuzi wa afisa mkuu mpya baada ya kubainika IEBC haikufuata sheria kabla ya kuwaorodhesha waliotuma maombi ya kuteuliwa kutwaa nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Ezra Chiloba.

Kampuni ya ushauri ya ACAL Ijumaa ilitia breki mchakato huo baada ya kueleza tume hiyo kwamba hawataki kazi hiyo hasa ikizingatiwa kandarasi kati yao na IEBC ilifaa kutiwa saini Ijumaa hiyo.

Kati ya sababu walizotaja kwa kuchukua hatua hiyo ni; kutohusishwa kuweka tangazo la kumtafuta mkuu mpya, maombi yaliyotumwa yaliangaziwa na usimamizi wa IEBC ilhali kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Marjan Hussein pia anamezea mate wadhifa huo na hata kudaiwa kusema matatizo yanayozonga tume hiyo kutokana na uchaguzi wa mwaka 2017 hayafai kutumika kuathiri utendakazi wake.

ACAL kukataa kuchukua kazi hiyo ni kati ya changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiandama IEBC katika juhudi zao za kupata mrithi wa Bw Chiloba.

Kati ya kampuni 11 IEBC ilikuwa imeorodheshwa kusaidia kumtafuta afisa mpya, ni nne pekee ziliwasilisha nia yao ya kutaka kupewa jukumu hilo. Nyingine saba kama PwC Kenya na Deloitte hazikuwasilisha ombi la kupewa jukumu hilo na hazikutoa sababu zozote za kutofanya hivyo.

Mnamo Alhamisi, IEBC ilichapisha majina ya watu 97 waliotuma maombi ya kutwaa wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji pamoja na majina 10 ya mwisho ya waliorodheshwa.

Kumi hao ni Dkt Joel Mabonga, Humphrey Nakitari, Mr Zephania Aura, Nancy Kariuki na Paul Kioko. Wengine ni Kaimu Afisa Mkuu mtendaji Marjan Hussein Marjan, Dkt Elishiba Murigi, Dkt Benjamin Tarus, Anne Mwasi na Dkt Billow Khalid.

Kujiondoa kwa ACAL sasa kunaibua maswali jinsi IEBC ilivyoibuka na majina 10 ya mwisho yaliyochapishwa Alhamisi na kampuni gani itakayoandaa mahojiano na wale walioorodheshwa.

Taifa Leo ilipofikia IEBC ili kusikiza kauli yao, ilielezwa kwa haibabaishwi na hatua ya ACAL na kusisitiza sheria inawapa makamishina wa sasa idhini ya kuteua afisa mkuu mtendaji.

“Tafadhali tambueni kwamba ni wazi katika sheria nani anafaa kuongoza mchakato wa kuteua afisa mpya mkuu mtendaji. Kutoa jukumu hili kwa ajenti ni kwa hiari tu na tume inaendelea na shughuli za kumteua afisa huyo. Wadau wote watajuzwa kuhusu hatua zilizopigwa jinsi tumekuwa tukifanya awali,” ikasema IEBC kupitia taarifa.

Ingawa kisheria si lazima kwa tume kumteua ajenti au kampuni kuongoza mchakato wa kuteua afisa mkuu mpya, IEBC imekuwa ikitumia kampuni kadhaa kuwapa kazi mameneja na wale wa nyadhifa za juu.

You can share this post!

KANU kujifufua kwa kufungua matawi mapya kote nchini

Polisi lawamani kwa kuteketeza nyumba tisa

adminleo