• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
Tanzania yatoa tahadhari kuhusu Ebola

Tanzania yatoa tahadhari kuhusu Ebola

NA MASHIRIKA

SERIKALI ya Tanzania Jumapili ilitoa tahadhari kuhusu maambukizi ya Ebola baada ya ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,400 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuripotiwa kusababisha vifo katika taifa jirani la Uganda.

Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu alitoa tahadhari hiyo kupitia akaunti yake ya Twitter na akaomba ushirikiano kati ya raia wa Tanzania na Uganda kwenye miji ya mipakani kuwa wenye umakinifu mkubwa.

“Ningependa kuwaarifu raia wa Tanzania kwamba kuna hatari ya ugonjwa wa Ebola kuenea hadi katika nchi yetu,” akasema Bw Mwalimu baada ya maafisa wa uhamiaji mpakani kukiri kwamba raia kutoka familia moja Uganda aliyekuwa amesafiri hadi DRC aliaga dunia Mashariki mwa nchi hiyo kutokana na Ebola.

Kulingana na Waziri huyo, wakazi wa miji ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania kama Kagera, Mwanza na Kigoma wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo unaoenea kama moto nyikani.

“Ingawa miji hiyo mitatu ipo hatarini, ni vyema kusema taifa lote liwe katika hali ya tahadhari kwa kuwa ugonjwa huo huenea haraka na husababisha vifo upesi,” akaongeza Bw Mwalimu.

Ili kudhihirisha kwamba Tanzania inapambana usiku na mchana kuhakikisha visa vya Ebola haviripotiwi nchini humo, Waziri Mwalimu siku ya Jumamosi alianza ziara katika maeneo ya mipaka na bandarini ili kukagua na kuweka mikakati maridhawa kuzuia tukio lolote la maambukizi ya Ebola.

Mnamo Ijumaa Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuwa mkurupuko wa Ebola haujafikia kiwango cha kutangazwa janga la kitaifa kiafya, kauli ambayo inafasiriwa kwamba Ebola bado inaweza kudhibitiwa kupitia uhamasisho na matibabu katika mataifa ambayo visa vyake vimeripotiwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) hutangaza magonjwa kuwa janga la kimataifa la kiafya iwapo utaenea hadi mataifa jirani na kuwaangamiza raia wengi.

Wiki jana mwanamke na mwanawe mwenye umri wa miaka mitano kutoka Uganda walifariki baada ya kupata maambukizi ya Ebola walipoenda kumtembelea mwanafamilia wao aliyekuwa akiugua Ebola nchini DRC.

Nduguye kijana huyo ambaye ana umri wa miaka mitatu tayari ameambukizwa Ebola huku wanafamilia wengine wakitengwa ili kuzuia ueneaji wa ugonjwa huo.

Hata hivyo, hakuna kisa chochote cha Ebola ambacho kimeripotiwa kuanzia Uganda kando na kile kilichowahusisha wanafamilia hao walioenda DRC kumtembelea mwanao aliyekuwa na maradhi hayo.

You can share this post!

Serikali yaonya wachochezi kwenye mzozo wa malisho

Njoo umchukue mtoto wako, lofa amzushia polo

adminleo