Kimataifa

Bashir aonekana mara ya kwanza tangu atimuliwe

June 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

KIONGOZI wa Sudan aliyeng’olewa madarakani, Omar el-Bashir mnamo Jumapili alionekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu ang’atuliwe.

Hii ilikuwa ni wakati alipofikishwa katika afisi ya kiongozi wa mashtaka jijini Khartoum akiwa chini ya ulinzi mkali.

Bashir alisafirishwa kutoka jela ya Kober, ambako amekuwa akizuiliwa, hadi afisi hiyo kuhojiwa na viongozi wa mashtaka kwa madai ya ufisadi.

Akivalia kanzu nyeupe, Bashir alikuwa chini ya ulinzi mkali wa magari ya maafisa wa usalama.

Alipofika katika afisi hiyo, Bashir alikuwa amezingirwa na maafisa wa usalama kila upande.

Aliposhuka katika gari alienda katika afisi hiyo akitabasamu na kuzungumza na maafisa waliokuwa wamemzingira.

Humo ndani alisomewa mashtaka yanayomkumba na akahojiwa na viongozi wa mashtaka.

Dakika chache baadaye aliondoka, japo bila tabasamu ya awali na akasafirishwa jela.

Mashtaka

Kiongozi wa mashtaka Alaeddin Dafallah alieleza wanahabari kuwa Bashir alifahamishwa kuwa anakumbana na mashtaka ya kumiliki sarafu za nchi nyingine, ufisadi na kupokea zawadi kinyume na sheria.

Bashir aling’olewa mamlakani Aprili 11 baada ya maandamano ya raia na jeshi likitwaa uongozi wa nchi tangu wakati huo.

Amekuwa akizuiliwa jela na hajaonekana mbele ya umma.

Kufikishwa kwake mbele ya viongozi hao wa mashtaka kulikuja wakati jenerali mmoja katika baraza la jeshi linaloongoza Sudan aliapa kuwa waliovamia waandamanaji nje ya makao mkuu ya jeshi mjini Khartoum na kuua watu mapema mwezi huu watahukumiwa kifo.

“Tunafanya juhudi kuwanyonga waliofanya hivyo. Yeyote aliyefanya kosa lolote ataadhibiwa,” akasema Mohamed Hamdan Dagalo, naibu mkuu wa baraza la kijeshi linaloongoza Sudan.