AUNTY POLLY: Kansa yaweza kusambazwa?
Na PAULINE ONGAJI
HIVI majuzi niligundua kwamba mwenzangu ambaye nimekuwa nikishiriki naye tendo la ndoa anaugua saratani ya matiti. Ni suala ambalo limenihuzunisha,na kunipa wasiwasi kuwa huenda hali yangu ya kiafya pia imo hatarini. Ningependa kujua je, naweza kuambukizwa kansa kwa kushiriki mapenzi na mwenzangu aliye na maradhi haya?
Jerald, 22, Mombasa
La hasha! Maradhi ya kansa hayawezi sambaa kupitia tendo la ndoa. Ugonjwa wa kansa hausambai kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kwa njia yoyote ile. Hata hivyo, virusi vya ‘Human Papillomavirus’ (HPV), vinavyosababisha kansa ya njia ya uzazi (Cervical Cancer) husambazwa kupitia njia hii. Aidha, kuna maradhi mengine ambayo waweza kuambukizwa kwa kushiriki tendo la ngono bila kinga kama vile Ukimwi, ‘Herpes’, ‘Hepatitis B’, kisonono na kaswende miongoni mwa mengine. Ndiposa unashauriwa kutumia kinga kila mara unaposhiriki ngono na yeyote hasa ikiwa uhusiano wenu haujarasimishwa.
Niko katika kidato cha pili ambapo majuma machache yaliyopita rafiki yangu wa karibu alifariki. Ni tukio lililoniacha na huzuni mwingi kiasi kuwa nimeshindwa kabisa kurejelea hali yangu ya kawaida. Ningependa kujua je, kuna tiba ya huzuni?
Ben, 16, Mombasa
Kwanza kabisa pokea risala zangu za rambirambi kwa kumpoteza mpendwa. Kwa kawaida huwa ni vigumu kujua jinsi ya kujidhibiti unapokumbwa na huzuni hasa katika umri wako. Ni vyema kwamba unajua nini hasa kinachokusababishia hisia hizi za huzuni. Ikiwa una rafiki wa karibu, zungumza naye au pia unaweza jadiliana na mtu mkomavu unayeamini. Utafiti unaonyesha kuwa viwango vya huzuni hupungua unapozungumzia suala lolote linalokutatiza. Aidha, waweza kusaka mawaidha kutoka kwa mshauri nasaha kwani mtaalamu huyu ana ujuzi wa kutosha kukupa mwongozo wa jinsi ya kukabiliana na tatizo hili. Mbali na hayo, jihusishe na shughuli zingine za kukusaidia kupunguza huzuni kama vile kucheza spoti, densi au kuimba. Aidha ningependa kukuambia kwamba, japo kifo huacha majonzi na uchungu, ni wazi kwamba kila nafsi sharti itaonja mauti, kumaanisha kwamba hili ni jambo ambalo haliwezi epukika. Itakusaidia ikiwa utaanza kukubali kwamba mwenzio ameenda na hatorudi tena.