• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
NTSA yashauri washikadau wa matatu

NTSA yashauri washikadau wa matatu

Na LAWRENCE ONGARO

HALMASHAURI ya usalama barabarani nchini (NTSA), imeweka mikakati jinsi ya kuendesha ukaguzi wa magari kwa njia ya uwazi.

Mkurugenzi wa NTSA, Bw Wilfred Okemwa, alisema Jumatatu mpango huo utaleta uwajibikaji kwa washikadau wote wa matatu na wamiliki wa magari ya kibinafsi.

Washikadau wa matatu na wadau wengine zaidi ya 150 walikongamana na wasimamizi wa NTSA mjini Thika ili kujadiliana kwa kina jinsi ya kukabiliana na baadhi ya changamoto zilizopo.

“Sisi lengo letu hasa ni kuona ya kwamba kila mmoja anatendewa haki bila kudhulumiwa na yeyote yule,” alisema Bw Okemwa, na kuongeza wangetaka kuwa na mikutano ya kila mara na washikadau ili kujadiliana yale yanayowahusu hasa zingatio likiwa ni maswala ya barabarani.

Jambo lingine muhimu alilosema ni kwamba vyombo vya habari viwe mstari wa mbele kuangazia mengi kuhusu jinsi NTSA inavyokabiliana na wenye magari barabarani.

“Iwapo watafanya hivyo bila shaka wananchi kule nje wataelewa ile kazi muhimu inayotekelezwa na NTSA hususan kukagua magari barabarani,” alifafanua Bw Okemwa.

Mkurugenzi wa NTSA Bw Wilfred Okemwa. Picha/ Lawrence Ongaro

Wakati wa mkutano huo washikadau waliohudhuria hafla hiyo walikuwa na maswali chungu nzima hukusu utendakazi wa NTSA na maafisa wa polisi.

Bw John Mwangi ambaye ni mshauri mkuu wa Mbunge wa Thika (Mhandisi Patrick Wainaina) alitaka kujua ni mbinu ipi NTSA itafuata kuona ya kwamba Polisi wa trafiki hawasumbui wamiliki wa matatu na wenye magari wakati wanapopeleka magari yao kwa ukaguzi.

Alipendekeza wao pia wapewe mafunzo maalum jinsi ya kukabiliana na maswala kama hayo kwa sababu wamekuwa wakinyanyasa wamiliki wa magari kote nchini.

Mhandisi wa NTSA kwa upande wa ukaguzi Bw Gerald Wangai, alisema vituo vya ukaguzi hapa nchini ni vichache kama 17 pekee na kwa mwaka moja wanastahili kukagua magari 3 milioni.

“Kwa mwaka mmoja vituo vya ukaguzi huweza kukagua magari 400,000 pekee,” alisema Bw Wangai

Alisema wanahimiza wajuzi wajitokeze ili kutafuta leseni ya kufungua vituo hivyo.

Alisema gari lolote litakuwa likifanyiwa ukaguzi wa kimitambo baada ya miaka minne, na hilo litakuwa ni jambo la lazima.

Alisema uchunguzi umebainisha kuwa magari madogo ndiyo yanayosababisha ajali nyingi barabarani na hiyo inatokana na maswala mengi.

Alisema iwapo kutatokea ajali, kuna mambo mengi yanastahili kuzingatiwa. Kwanza, ni vyema kuelewa iwapo kiwanda kilichounda gari hilo kilizingatia masharti yote ya kuunda gari. Halafu, aliyekagua gari hilo na kulipitisha kuwa gari liko sawa pia anastahili kuwajibishwa.

Washikadau pia walidai kuwa ajali za barabara zinatokea kutokana na ukosefu wa alama za barabara hazipo na pia barabara zenyewe ni mbovu.

Mwenyekiti wa wamiliki wa matatu mlima Kenya Bw Michael Kariuki aliwanaohusika na vidhibiti mwendo vya magari wawe na msimamo mmoja badala ya kila mara kuwahangaisha kwa kutaka wabadilishe vifaa hivyo.

“Sisi kama washikadau tumehangaishwa kwa muda mrefu kwa kuagizwa kila mara kubadilisha vidhibiti kasi. Kwa hivyo, tunataka NTSA kuingilia kati ili kuchunguza jambo hilo,” alisema Bw Kariuki.

You can share this post!

Suarez awatambisha Uruguay dhidi ya Ecuador kwenye Copa...

‘Wanaotaka kura za Mlima Kenya watangaze ni jinsi...

adminleo