• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Hujatwambia Raila aliokoka, Kimani Ngunjiri amjibu Rais

Hujatwambia Raila aliokoka, Kimani Ngunjiri amjibu Rais

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Bahati Kimani Ngunjiri amezidi kutetea hatua yake pamoja na viongozi wengine wa Jubilee kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto, na kuendelea kupinga muafaka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Bw Ngunjiri Jumatatu alisema kuwa kama viongozi wanaotambua muungano baina ya Rais na naibu wake William Ruto pekee, bado wanafuata ushauri aliowapa Rais kuwa Bw Odinga si mtu mzuri, na hivyo hawajui vingine.

Alishangaa ni kwa nini Rais anawakashifu katika runinga kwa kumkosoa Bw Odinga, badala yake akimtaka kuitisha mkutano wa chama ili awape sababu za kumkumbatia kiongozi huyo, ambaye alikuwa hasimu wa Rais kabla ya muafaka wa Machi 9, 2018.

“Handisheki ya 2013 ndiyo mimi naamini, ile ya Ruto na Uhuru. Wewe tuite utuambie huyu mtu (Raila) si kimundu, si mkora (jinsi walikuwa wakimwita), utuambie ni mtu mzuri sasa. Wewe hujatuambia kama aliokoka,” akasema mbunge huyo, ambaye alikuwa akizungumza katika mazishi ya kakake.

Alisema hawawezi kulazimishiwa kukubali handisheki, ila sharti Rais awaite na kuwaeleza manufaa yake.

“Wakati unazungumza nasi katika runinga, nasi kujibu katika runinga, wanaofaidika ni wale (ODM). Hata hii handisheki usitusukumie, uache tuikague, tuite mkutano wa wabunge utueleze kuihusu,” Bw Ngunjiri akasema.

Alikuwa akizungumza siku moja tu baada ya Rais Kenyatta kuwaonya viongozi kutoka ngome yake ambao wamekuwa wakikaidi amri zake na kuzunguka nchini wakifanya siasa, badala ya kazi.

Rais aliwaita viongozi hao Wakora na Uchafu, na akasema atawatoa kila walipojificha. Alisema hawataenda popote bila msaada wake.

You can share this post!

Ruto aahidi kutatua mzozo wa wabunge na maseneta

Kaunti zipewe fedha kukabiliana na Ebola – Maseneta

adminleo