Habari MsetoSiasa

Kaunti zipewe fedha kukabiliana na Ebola – Maseneta

June 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

MASENETA Jumanne waliitaka Serikali Kuu kuchukua hatua za haraka kutoa pesa inazodaiwa na serikali za kaunti, ili zijiandae kukabiliana na majanga ya kiafya yanayoweza kuzikumba, kama tishio kuhusu ugonjwa wa Ebola ambalo lilikumba Kaunti ya Kericho.

Maseneta wa Kamati ya Afya walisema kuwa hakujakuwa na umakinifu wa kutosha kwa serikali kukagua watu wanaoingia nchini kuhakikisha kuwa hawajaathirika na magonjwa yanayoweza kuhatarisha wengine na wakaitaka Wizara ya Afya kuhakikishia Wakenya kuwa inafanya ukaguzi inavyostahili.

Aidha, maseneta hao walisema serikali za kaunti haziko tayari kukabiliana na majanga ya dharura yanayoweza kuzikumba kimatibabu, kwa kuwa hazina pesa za kufanya hivyo.

“Tunashangaa ikiwa Kaunti ya Kericho ilikuwa tayari kukabiliana na kisa cha jana (Jumatatu), ikiwa ingeibuka kilikuwa cha Ebola, kaunti hiyo ilikuwa tayari kukikabili kweli?” akauliza mwenyekiti wa kamati hiyo Michael Mbito.

Seneta Maalum Beth Mugo alisema kaunti zinahitaji kupewa pesa zaidi ili kuziwezesha kujikinga kutokana na magonjwa hatari kama Ebola, akisema kwa sasa hazina uwezo huo.

Seneta Naomi Masitsa aidha alipendekeza Serikali Kuu na za kaunti ziwe zikishirikiana kila wakati kufanya ukaguzi, na kaunti ziwezeshwe kifedha ili kukabiliana na mavamizi yoyote ya magonjwa.

Viongozi hao walisema tofauti baina ya Seneti na Bunge la Taifa kuhusu mgao wa fedha kutoka kwa Serikali Kuu hadi kwa zile za kaunti aidha zimesababisha kaunti kukosa pesa ambazo zingezisaidia kukabiliana na majanga.

Ujumbe wao ulikuja siku moja tu baada ya Baraza la Magavana (CoG) kulalamika kuwa hadi sasa serikali bado haijatuma pesa nyingi kwa serikali za kaunti (Sh5 bilioni ambazo zinafaa kwenda katika sekta ya afya).