Habari Mseto

Jowie akumbushwa maskani yake ni rumande

June 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MPENZIWE aliyekuwa mtangazaji wa runinga Jacque Maribe, Bw Joseph Kuria Irungu almaarufu Jowie ataendelea kukaa gerezani baada ya ombi lake la pili la kuachiliwa kwa dhamana kukataliwa na mahakama kuu Jumanne.

Jaji James Wakiaga alitupilia mbali ombi la Jowie akisema “hakujakuwa na mabadiliko tangu aliponyimwa dhamana mara ya kwanza.”

Akikataa ombi la Jowie, Jaji Wakiaga alisema usalama wa mashahidi ungali unapewa kipa umbele na mshtakiwa hawezi kuachiliwa kwa dhamana kwa wakati huu.

“Usalama wa mashahidi unazingatiwa na mshtakiwa ambaye ni tisho kwa hawezi kuachiliwa kwa dhamana kwa sasa hadi pale watakapotoa ushahidi mahakamani,” alisema Jaji Wakiaga.

Jaji alisema ombi hilo la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana litafikiriwa upya baada ya mashahidi wanne wanaolindwa na Serikali wakikamilisha kutoa ushahidi wao dhidi yake.

Mahakama ilisema ripoti ya urekebishaji iliyotolewa inapendekeza mshtakiwa asiachiliwe kwa dhamana kwa sasa.

“Ombi la mshtakiwa la kuachiliwa kwa dhamana itafikiriwa upya baada ya mashahidi wanaolindwa kutoa ushahidi,” alisema Jaji Wakiaga..

Kesi dhidi ya wapenzi hao itaanza kusikizwa wiki ijayo.