• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
Serikali yaongeza juhudi za kujikinga kutokana na Ebola

Serikali yaongeza juhudi za kujikinga kutokana na Ebola

GEORGE ODIWUOR na VITALIS KIMUTAI

WATU wanne waliolazwa katika hospitali ya rufaa ya Kericho kwa hofu kuwa wanaugua Ebola wataondolewa katika wodi ambapo walikuwa wamefungiwa na kutangamana na wagonjwa wengine, baada ya uchunguzi waliofanyiwa kuonyesha kuwa hawana ugonjwa huo.

Waziri wa Afya kaunti hiyo Shadrack Mutai alisema wagonjwa hao pia watapewa ushauri nasaha kutokana na woga walioingiza kwamba labda wameambukizwa. “Watapelekwa katika wadi walipo wagonjwa wengine wakiendelea kukaguliwa na madaktari, baada ya matokeo ya uchunguzi wa shirika la utafiti wa kimatibabu (KEMRI) kuonyesha hawana Ebola,” akasema Dkt Mutai.

Aliwataka majirani na familia za wagonjwa hao kuwapokea tena watakapopata nafuu, kwa kuwa wamebainika kuwa sawa.

Mwanamke aliyekuwa amesafiri hadi Kericho kumwona mpenzi wake kutoka Malaba, Kaunti ya Busia alikimbizwa katika hospitali ya Siloam kabla ya kupelekwa katika ile ya rufaa ya Kericho Jumapili, akiwa na dalili sawa na za wagonjwa wa Ebola.

Mumewe na watu wengine wawili waliompeleka hospitalini mnamo Jumatatu walifungiwa katika wodi moja iliyotengwa kama mbinu ya kuzuia usambazaji, wakati uchunguzi wa kimatibabu ulikuwa ukifanywa na shirika la KEMRI kubaini ikiwa walikuwa wameathirika.

Wakati huo huo, maafisa wa afya katika Kaunti ya Homa Bay wameanza kuwakagua wanaotumia boti katika Ziwa Victoria, wakati serikali inazidisha juhudu za ukaguzi dhidi ya Ebola nchini.

Idara ya Afya Homa Bay imeweka vituo vya ukaguzi visiwani Ziwa Victoria, ili kukagua watumizi wa boti wanaotoka Uganda, kutokana na tishio la Ebola.

Kuzidishwa kwa juhudi hizi ni kutokana na mkurupuko wa ugonjwa huo nchini Uganda. Kaunti ya Homa Bay inapakana na Uganda na Tanzania ziwani, ambapo watu wengi hutumia boti kuingia na kutoka nchini, mara nyingi bila kukaguliwa.

Maafisa wa afya jana walianza kukagua watu katika visiwa vya Mfangano, Remba, Ringiti na Kiwa, ambavyo hupokea watu wengi kutoka Uganda, hivyo vikionekana kuwa hatarini kwa maambukizi ya virusi vya Ebola nchini.

Maafisa wengine wa ukaguzi watapiga kambi katika miji ya Sindo na Mbita, ambapo wafanyabiashara katika mataifa haya mawili hupitia sana.

Waziri wa Afya kaunti hiyo Richard Muga alieleza wanahabari kuwa wizara ya afya kitaifa ilitahadharisha kaunti kuwa makini katika maeneo hayo, punde tu kisa cha Kericho kiliporipotiwa.

“Hatujathibitisha kisa chochote cha Ebola nchini lakini kutokana na hali kuwa tuko karibu na Uganda ambapo visa hivyo vimethibitishwa, sharti tuwe makini zaidi kuzuia mkurupuko. Tutakagua wasafiri, wavuvi, wafanyabiashara na yeyote anayesafiri kutoka Uganda ambapo ugonjwa huo umethibitishwa,” akasema Profesa Muga.

Wodi za kufungia wale wanaohofiwa kuambukizwa ugonjwa huo tayari zimetengwa na vifaa kutumwa kutoka Nairobi, kama matayarisho endapo kutatokea kisa kitakachoshukiwa kuwa cha Ebola.

Serikali Kuu aidha inakagua watu wanaoingia nchini mipakani na katika viwanja vya ndege.

You can share this post!

Ufisadi ni hatari kuliko Ebola – Wabukala

Ruto kuishtaki HELB kuhusu mikopo

adminleo