• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Ruto kuishtaki HELB kuhusu mikopo

Ruto kuishtaki HELB kuhusu mikopo

NA VITALIS KIMUTAI

KINARA wa Chama cha Mashinani (CCM), Bw Isaac Ruto, amewataka mawakili kuwasilisha kesi mahakamani kupinga hatua ya Bodi ya Kutoa Mikopo ya Elimu ya Juu(HELB), kuwanyima fedha wanafunzi ambao hawajapata kitambulisho cha kitaifa.

Bw Ruto alisema HELB inaendeleza ubaguzi na kukiuka haki za wanafunzi wa vyuo na taasisi za elimu kwa kuwanyima mkopo huo muhimu kutoka kwa serikali.

“Nimewaeleza mawakili waelekee mahakamani na kupinga hatua ya HELB kwa kuwa hili ni suala linalohusisha umma. Hii ni kwasababu mamia ya wanafunzi wametueleza kwamba wanahukumiwa kwa makosa ambayo si yao,” akasema Bw Ruto.

Gavana huyo wa zamani wa Bomet, alisema mamia ya wanafunzi wanaokamilisha kidato cha nne huwa hawajahitimu umri wa kupata kitambulisho, huku wengine wanaotuma maombi wakisubiri kwa muda mrefu kabla ya kupata stakabadhi hiyo.

Alisema hayo baada ya kukutana na wanachama wa Chama cha Mawakili (LSK) tawi la Kusini mwa Bonde la Ufa, walioongozwa na mwenyekiti wao, Bw Kipngetich Korir nyumbani kwake Tumoi, eneobunge la Chepalungu.

Majuzi, Afisa Mkuu Mtendaji wa HELB , Bw Charles Ringera akiwa mjini Bomet,alilalamika kwamba bodi hiyo ilipoteza zaidi ya Sh6.6 bilioni kwa kukosa data ya wanafunzi 64,000 waliosoma kati ya 1974 na 1979 kwa kuwa hawakuwa na vitambulisho.

You can share this post!

Serikali yaongeza juhudi za kujikinga kutokana na Ebola

IEBC isalie na makamishna saba, KNHRC yapendekeza

adminleo