Makala

VITUKO: Mzee Pengo atua Bushiangala akitumai kurina vya Asumini

June 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMUEL SHIUNDU

“UTAFURAHIA kukutana naye” Pengo alihakikishiwa kwa mara ya ngapi sijui, “Si Ukarimu ule aliojaliwa. Sikwambii sura yake nzuri. Nasikia yuko duniani kimakosa kwani alipoumbwa alikusudiwa kuwa malaika wa peponi.” Sindwele aliendelea kumfafanua Asumini.

Bahati haikuwa naye. Hakufanikiwa kumwona kiumbe huyo wa peponi.

Ilisadifu kwamba siku hiyo ambayo Sindwele alimleta kwa malaika huyu karimu, malaika mwenyewe alikuwa kaenda kushughulikia mengine.

Sindwele alikuwa kajuzwa na Simba kwamba walimu wakuu walihitaji muda zaidi katika mkutano wa kitaifa wa walimu wakuu kule pwani.

Sindwele akajiambia kwamba huo ungekuwa wakati mwafaka wa kushiriki mazungumzo ya karibu na binti huyo bila uwepo wa Simba.

Ulikuwa wakati wake wa kutawala baada ya kuondoka kwa panya.

Akaiteua siku hii kuandamana na Pengo ili naye akalione hilo ua la asumini.

Kwenye mlango wa kibanda cha Asumini, walipata tangazo kwamba, ‘kutokana na sababu ambazo hazingeepukika hapangekuweko na huduma’.

Pengo alishangaa ni huduma gani hizo ambazo Asumini aliwapa akina Sindwele hadi wakawa wanamlinganisha na malaika wa peponi.

“Sijui kwa nini anaishi hapa Bushiangala, angeweza kwenda kuigiza filamu maarufu huko Ulaya” Pengo alikumbuka jinsi Sindwele alikuwa kambwambia siku ya kwanza alipomfichulia majilio ya kipusa huyu hapo kijijini.

Mawazo mengine kichwani

Huku Pengo akiyawazia hayo, mawazo tofauti yalimpita Sindwele kichwani.

Alishangaa iwapo Simba naye alikuwa miongoni mwa hizi sababu ambazo hazingeweza kuepukika.

Aliamini kwamba shule ziliwafaidi walimu wakuu, na mradi Simbamwene mwenyewe angali katika fukwe za miji ya pwani, yeye Sindwele hakuwa na sababu yoyote ya kumrejesha shuleni baada ya kutamatika kwa likizo fupi.

Baada kuikosa fursa hii adimu ya kuliona ua hilo lililosifiwa na Sindwele, Pengo akaamua kuelekea makao ya tume ya huduma kwa walimu kushughulikia marupurupu yake ya mazingira magumu ya kazi.

Tangu kuhamia shule ya upili ya Sidindi, hajayapokea marupurupu haya japo shule hiyo ilikuwa katika eneo lililotengewa marupurupu hayo. Alipowasimulia rafiki zake kuhusu kucheleweshewa marupurupu haya, walimwambia kuwa huko Sidindi hakukuwa na ugumu kama ule uliokuwa katika shule uchwara kama Maka.

“Hayo marupurupu mnapewa ya kazi gani bwana?” mwalimu Soo aliwahi kumsaili siku moja.

Pengo alikubaliana na Soo kwamba kule Maka na Bushiangala ndiko kulikopaswa kutengewa marupurupu ya mazingira magumu, lakini angefanyaje na bahari hakuitia chumvi yeye? Hakuwa na ujasiri wa kuyakataa marupurupu hayo. Aliwashauri wenzake wapambane na hali zao.