• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Vijana wapatao 30 wazindua biashara ya kuchonga viazi Thika

Vijana wapatao 30 wazindua biashara ya kuchonga viazi Thika

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA wapatao 30 mjini Thika wamezindua mradi wa kuchonga viazi na kuuzia wateja wao.

Vijana hao wanaojiita Jungle Investors, wanasema walihimizwa kufanya biashara hiyo na Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina, kama njia mojawapo ya kudhihirisha si lazima mtu asubiri kuajiriwa afisini.

Bw Wainaina alisema Jumanne furaha yake ni kuona vijana waliokamilisha elimu katika viwango mbalimbali wanajizatiti na kuingilia kazi za kujiajiri wenyewe bila kutegemea kupewa hizo kazi.

“Ninataka kuona vijana wengi wakijitokeza na ubunifu wa ajira tofauti. Mimi kama mbunge wa eneo la Thika niko tayari kuona ya kwamba ninapigania kuona ya kwamba wanapata fedha chache za Uwezo Fund ili wajitegemee kabisa,” alisema Bw Wainaina.

Kulingana na mbunge huyo, vijana hao walizindua mradi huo mwaka moja uliyopita na tayari wamepiga hatua kubwa ajabu.

“Mimi lengo langu ni kuona ya kwamba tunafuata ajenda nne za serikali ambapo mojawapo ni ajira kwa vijana. Iwapo vijana watafuata mkondo wa kujitegemea bila shaka tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwa upande wa ajira,” alisema Bw Wainaina.

Anatoa mwito kwa vijana kujitokeza kwa wingi ili kujitegemea kiajira, na yeye yuko tayari kuwapiga jeki iwapo watajiweka kwa vikundi vya watu 10 au zaidi.

Kupiga hatua kifedha

Alisema kulingana na kazi hiyo kila mmoja huweza kupata Sh1,500 kila siku jambo alilosema ni kupiga hatua kubwa kifedha.

Bi Mary Wanjiku ambaye ni mmoja wa vijana wanaoendesha mradi huo anasema sasa ni mwaka mmoja hivi tangu wajitokeze wazi kuchonga viazi na kuuzia wateja wao.

“Kazi imekuwa nzuri ajabu ambapo kwa wakati huu tumepata mteja mkuu katika mkahawa mmoja mjini hapa na tayari wakati huu tunatarajiwa kupeleka zaidi ya kilo 1,000 ya viazi vilivyochongwa vyema,” alisema Wanjiku.

Alisema kwa siku moja wana uwezo wa kuchonga viazi zaidi ya kilo 100 pekee, na kwa hivyo wanastahili kukaza buti zaidi ili kutosheleza wateja wao.

Biashara ya kuchonga viazi na kuwauzia wateja yanoga Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema kilo moja ya viazi vilivyochongwa ni Sh 100 na tayari wateja wengi wameanza kufurika katika maskani yao ili kununua viazi hivyo.

Alisema viazi hivyo wao huvitoa katika kaunti ya Nyandarua na kuvisafirisha hadi Thika.

Baadhi ya mitambo wanayotarajia kununua zaidi ili kurahisisha kazi hiyo ni ile ya kuchonga, kukausha na kuweka alama za bidhaa hiyo.

Alisema tayari wana mtambo wa barafu ambao unaweza kuhifadhi viazi hivyo kwa zaidi ya mwezi mmoja bila kuharibika.

You can share this post!

Msichana achomwa na mama mzazi kwa kuchelewesha nyanya

Mshukiwa wa wizi Zimmerman anusurika kifo

adminleo