• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Mabadiliko kushuhudiwa katika masomo ya shule za sekondari

Mabadiliko kushuhudiwa katika masomo ya shule za sekondari

Na OUMA WANZALA

SERIKALI imeanzisha rasmi mchakato wa kuandaa mtaala mpya wa masomo ya shule za upili. Hii ni kufuatia mkutano wa wiki jana uliowashirikisha wadau wa elimu mjini Naivasha.

Wataalamu katika sekta ya elimu wanatarajiwa kuanzisha safari ya kuunda mtaala huo, ambao utaleta mageuzi makubwa kuhusu namna wanafunzi wanavyofundishwa. Kulingana na mabadiliko hayo, elimu ya sekondari itaanza katika darasa la saba, ambalo litajulikana kama Gredi ya Saba na kukamilika katika kidato cha nne.

Wakati wa mkutano wa wiki jana, ilibainika kwamba mtaala mpya wa shule za sekondari utajumuisha masomo 25 na wanafunzi watachagua masomo yasiyopungua 12 na kuongeza mengine kwa hiari.

Vilevile ni katika kiwango hiki ambapo talanta za mwanafunzi na masomo wanayochangamkia yatatambuliwa, kisha waruhusiwe kujikita katika masomo hayo pekee.

“Wanafunzi watachagua kujikita katika vitengo vitatu; michezo na masomo ya mazoezi, elimu ya kijamii na masomo ya jumla yanayohusu Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu,” ikasema ripoti ya wataalamu waliokutana mjini Naivasha wiki jana.

Badala ya mtihani wa kitaifa kutumika kama kigezo cha kuwapima wanafunzi, watakuwa wakitunukiwa alama katika masomo yote watakayokuwa wakishiriki na alama hizo zitachangia matokeo ya mwisho watakayoyapata baada ya kukamilisha masomo yao.

Hata hivyo, mtihani wa kitaifa bado utakuwa ukifanyika ila utachangia tu asilimia 30 ya matokeo ya jumla ya kila mwanafunzi.

“Wanafunzi watakuwa wakikaguliwa na kupewa alama katika masomo yao na walimu wao. Ripoti ya matokeo itakayotolewa na walimu itachangia asilimia 70 ya alama za jumla huku mtihani wa kitaifa utakaoandaliwa na KNEC ukichangia asilimia 30,” ikasema ripoti kutoka kwa Taasisi ya Kuandaa Mtaala Nchini (KICD).

“Wanafunzi watatuzwa alama kwa kuzingatia iwapo wamezidi, wametimiza, wamekaribia au wamekosa kutimiza matarajio ya walimu wao na silabasi,” ikaongeza ripoti ya KICD.

Kupita mtaala mpya, jukumu la walimu litabadilika kutoka kufundisha hadi kutoa mwongozo na kuwasaidia wanafunzi kufahamu mambo kuhusu masomo yao, badala ya kukwamilia tu yaliyomo kwenye mtaala jinsi ilivyo sasa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KICD, Dkt Julius Jwan aliwataka wataalamu hao kuongeza bidii katika kubuniwa kwa mtaala huo ili kuzuia kikimbiza mambo dakika za mwisho mwisho.

“Waziri wa Elimu ametuagiza tujipange na kumaliza masuala yote kwenye mtaala huu ili kuzuia kuharakisha kutimiza malengo jinsi ilivyokuwa kwenye CBC ya wanafunzi wa shule za msingi.

Natarajia mtakuwa tayari wakati wowote kutekeleza awamu mbalimbali za mtaala huu pindi tu zitakapokuwa tayari,” akasema Bw Jwan.

You can share this post!

Gor Mahia Youth, Butterfly na Tandaza zawika

Somo la usalama barabarani kuanza kufundishwa

adminleo