• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vikatizi vya mawasiliano bora na madhara yake

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vikatizi vya mawasiliano bora na madhara yake

Na MARY WANGARI

BAADHI ya vikatizi vya mawasiliano bora ni:

  • kutokuwa na ujuzi wa kutosha wa lugha fulani
  • matamshi mabaya ya maneno
  • kutozingatia kaida za lugha, kwa mfano, katika maamkuzi
  • kutumia ishara vibaya
  • tofauti za kiumri.Kutoelewa mada vizuri
  • masafa marefu baina ya wanaowasiliana
  • uhusiano wa mbali baina ya wanaowasiliana
  • kuwa na hisia kupindukia
  • kuharibika kwa mtambo wa mawasiliano
  • kelele

Madhara yanayotokana na kukatizwa kwa mawasiliano

Haya hapa baadhi ya madhara yanayotokana na kukatizwa kwa mawasiliano bora:

Kukatizwa kwa mawasiliano baina ya wazungumzaji.

Hufanya ujumbe fulani kutoeleweka vizuri.

Huzua hali ya kutoelewana baina ya watu.

Huchelewesha kupokelewa kwa ujumbe.

Huweza kuzua hali ya kutoelewana baina ya watu.

Kugharimika kwa bure tu katika mawasiliano – rununu.

Makosa katika matumizi ya lugha

Makosa ya lugha hutokea pale ambapo mtumiaji wa lugha hutamka au kuandika maneno bila kuzingatia kanuni zinazotawala lugha.

Vyanzo vya makosa ya lugha

Athari za lugha mama

Athari hutokea lugha mama inapoingiliana na lugha ya Kiswahili.

Matokeo ni kuwa kanuni za kisarufi hukiukwa na sauti za Kiswahili kutamkwa aukuandikwa vibaya. Huenda mpangilio wa sauti katika lugha ya kwanza ukagongana na ule wa lugha ya Kiswahili.

Kwa mfano, kuna lugha ambapo sauti /b/ haiwezi kutokea bila ya kutanguliwa na /m/.

Aghalabu iwapo wazungumzaji wa lugha kama hii watakutana na lugha ambapo sauti /b/huweza kutokea bila kutanguliwa na /m/, watu hawa wataathirika wanapokutana na maneno yenye sauti /b/.

Bila shaka wataongezea /m/.

Kwa mfano,

baba kutamkwa kama mbamba

bure kuwa mbure

bora kutamkwa mbora

Kila lugha huwa na sauti zake mahususi ambazo zinaweza kuchukuana au kutofautiana na lugha ya pili. Kwa hivyo, huenda sauti fulani ikapatikana katika Kiswahili lakini isipatikane katika lugha ya kwanza ya anayejifunza Kiswahili.

Mara nyingi wengi hushindwa kuitamka na hivyo kuidondosha au kukimbilia sauti iliyokaribiana nayo kimatamshi.

Mifano:

Kosa                      Sahihi

 yuu                          juu

mbalambala          barabara

roo                            roho

zahabu                    dhahabu

mtoko                     mdogo

 

[email protected]

Marejeo

Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.

Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.

Maddo, U. & Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publishers.

You can share this post!

AFCON 2019: Fahamu vikosi vya timu zinazoshiriki

Shughuli ya kukarabati barabara za mashinani yaendelea...

adminleo