Makala

KIKOLEZO: Wamekanyagiwa sana Hollywood

June 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na THOMAS MATIKO

KULINGANA na ripoti mbalimbali za kule majuu, mojawapo ya sifa muhimu unayotakiwa kuwa nayo ili uweze kutoboa Hollywood, ni mwonekano wenye mvuto.

Haijalishi kipaji chako cha uigizaji. Sura ni kiungo muhimu sana kwa mwigizaji yeyote anayesaka ulaji Hollywood. Na hata mbaya zaidi inapokuwa ni mwigizaji wa kike.

Hii ndiyo sababu kumekuwepo na ripoti za ubaguzi Hollywood kwa misingi ya ni mwigizaji bora tu anayestahili kupewa kazi hasa kwa upande wa mademu ila wapo wale wanaoonekana kupendelewa kutokana kuhusishwa kwenye idadi kubwa za filamu.

Pia wapo wale ni wazuri, wana vipaji ila kwa sababu moja au nyingine vipaji vyao huwa havidhaminiwi sana licha ya kuonyesha uwezo wao.

Hawa ni baadhi ya waigizaji shupavu ambao michango yao huchukuliwa kuwa ya kawaida sana. Hawathaminiwi.

JENNIFER LOPEZ

Jennifer Lopez. Picha/ Hisani

Japo umaarufu wake mkubwa umetokana na muziki, J-Lo pia ni miongoni mwa waigizaji stadi wa kike ambao hawajapata shavu inavyotakiwa.

J-Lo amekuwa akiigiza kwa miaka mingi sana tangu miaka ya themanini na baadhi ya filamu zake zimefanya vizuri kwa mfano The Boy Next Door, The Wedding Planner na Monster in Law.

Licha ya kukosa utambuzi, hajawahi kufa moyo au kuchoka na ameendelea kuzidi kutisha ajuavyo yeye. Filamu yake mpya ni Second Act (2018).

GABRIELLE UNION

Ni mwigizaji mwingine wa kike ambaye hajapata heshima yake. Filamu iliyotangulia kumtoa ni Men In Black (1997) alikoigiza kama mke wake Will Smith.

Filamu hiyo iliishia kuuza zaidi ya dola 200 milioni ilipotoka miaka hiyo. Toka kipindi hicho mpaka sasa Gabrielle ameendelea kuigiza akitokea kwenye filamu na ‘series’ maarufu kama vile Being Mary Jane, Bring It On, Breaking In, Daddy’s Little Girl miongoni mwa zingine kibao. Kaorodheshwa mara kadhaa miongoni mwa waigizaji wa kike wenye asili ya mtu mweusi wanaolipwa mshahara mkubwa.

Hata hivyo kipaji chake kimeendelea kuonekana cha kawaida sana kuhusishwa kwenye filamu kubwa kubwa zaidi, nyingi akitumika kama mwigizaji mshirikishi/msaidizi.

ANGELA BASSETT

Akiwa na umri wa miaka 60 Angela ameendelea kusumbua kwenye ulingo wa uigizaji.

Kinachoumiza ni kwamba japo ni maarufu, sio wengi mashabiki wa filamu wanaweza kumtambua.

Lakini sio hao tu, hata Hollywood licha yake kuitumikia kwa zaidi ya miongo mitatu, bado anaonekana kuchukuliwa kuwa mwigizaji wa levo ya kawaida sana.

Angela Bassett. Picha/ Hisani

Wengi wamepata kumfahamu Angela kutokana na uhusika wake kwenye filamu ya Black Panther alikoigiza kama Ramonda.

Mbali na mafanikio ya filamu hiyo, hajaanza leo.

Aliwahi kuigiza kwenye filamu ya Malcom X akiwa na staa Denzel Washington.

Uigizaji wao uliishia kuishindia filamu hiyo tuzo ya Oscar.

Hata hivyo, huwezi kulinganisha mafanikio yake na ya Denzel anayethaminiwa sana kikazi.

REGINA KING

Ni mwigizaji mwingine mweusi aliyeitendea haki tasnia ya uigizaji kwa kupambania nafasi kwenye meza ya mapebari.

Haijalishi hawamtathamini, ila kazi yake ni kubwa na kila mmoja anajua. Hapa unamzungumzia mwanamke wa kike ambaye uhusika wake mara nyingi katika filamu umekuwa wa utetezi wa haki. Regina kacheza kwenye filamu ya If Beale Street Could Talk (2018) iliyofanya vizuri sana mada yake ikiwa ni ubaguzi wa rangi. Pia kacheza kwenye ‘series’ ya Left Over, kahusika kwenye utengenezaji wa ile ya Scandal na zingine kibao. Licha ya bidii yake, shavu bado kakaushiwa akichukuliwa kuwa wa kawaida mno.

THANDIE NEWTON

Ni mwigizaji mwingine ambaye licha ya kuwa na kipaji kikubwa na kujituma sana, bado thamani yake inaonyeshwa kuwa ndogo.

Kaonyesha uwezo wake kwenye ‘series’, filamu na drama za televisheni. Kwa wanaomtambua kikweli, wanamkubali.

Thandie alianza kuigiza akiwa na miaka 19 alipotokea kwenye filamu yake ya kwanza Flirting (1991).

Kadri miaka ilivyozidi naye akazidi kuboreka akihusika kwenye filamu kibao. Mission Impossible II, Beloved, The Chronicles of Riddick ni baadhi tu ya kazi kubwa alizohusika.

Hata hivyo mara nyingi amekuwa akipewa uhusika wa mwigizaji msaidizi/mshirikishi, kitu ambacho hakijazima nyota yake ila kimemkingia kuboresha thamani yake.

ALYSSA MILANO

Ni mrembo na anacho kipaji hatari. Amekuwepo kwa miaka mingi sasa ila sio wengi wanamtambua.

Sio kwa sababu hafanyi kazi nzuri, ni kutokana na yeye kutothaminiwa na kuwekwa katika nafasi anayostahili na wadau wanaohusika.

Imemchukua Alyssa mwenye miaka 46 zaidi ya miongo mitatu kuanza kupata kazi anazotokea kama muhusika mkuu. Kwa miaka mingi ametumika kama mwigizaji msaidizi. Japo hili linaonekana kubadilika kidogo katika miaka ya sasa, ni ishara kamili ya jinsi hajakuwa akithaminiwa na wadau kwenye fani.