MAWAIDHA YA KIISLAMU: Zoea kujihesabu nafsi yako kabla ya hesabu kali Siku ya Kiyaamah
Na HAWA ALI
KILA sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wata’ala) Muumba wa wanaadamu na kuwaekea mauti yawe ni mtihani kwao ili kuwabainisha ni nani kati yao atakayefanya ‘amali nzuri. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).
Ndugu wa Kiislamu, hakika ni jambo lisilo na shaka yoyote kwa Muumin kuwa baada ya maisha haya tuliyonayo hapa ulimwenguni kuna maisha mengine ya milele huko akhera.
Kuliamini hili ni nguzo katika nguzo sita za imaan. Na inajulikana kuwa katika maisha ya akhera kutakuwa na hali mbili tu, ima ni maisha mazuri na yenye starehe za kudumu kwa waliofuzu au maisha ya dhiki, tabu na adhabu juu ya adhabu kwa walioshindwa kufuzu.
Kufuzu kwa mja kutalingana na hesabu ya matendo yake, hesabu ambayo itakusanya kila alilolifanya kubwa au dogo kama anavyothibitisha Allah (subuhanahu wata’ala) kwa kusema: “Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu.” [Al-Anbiyaa (21) : 47].
Ndugu wa Kiislamu, kwa vile kila mmoja wetu anapendelea awe miongoni mwa watakaopata maisha ya raha na starehe huko akhera, ni vyema tukaanza kujihesabu wenyewe kabla ya kuja kuhesabiwa matendo yetu na Allah (subuhanahu wata’ala), kama ilivyo kawaida ya mwanafunzi anayejiandaa kuufanya vizuri mtihani wake wa mwisho huwa anajitathmini kwa kufanya mitihani midogo midogo na kujipima uwezo wake.
Amirul Muuminina Sayidna Omar ibn Alkhatwab (radhi za Allah ziwe juu yake) ametuusia kwa kusema: “Hesabuni nafsi zenu kabla ya kuhesabiwa, na zipimeni kabla ya kupimwa, kwani ni bora (wepesi) kwenu kupima (amali zenu) leo kabla ya (kupimwa) kesho kwenye Hesabu, na jipambieni kwa siku ya Hadhara kuu, “Siku hiyo mtahudhurishwa haitafichika siri yoyote.” [Al-Haaqah (69) : 18].
Hivyo ni juu ya kila mmoja wetu kuanza kuitathmini nafsi yake na kuyahesabu matendo yake ya kila siku anayoyafanya, je yako upande gani? Ni katika yale anayoyaridhia Allah (subuhanahu wata’ala) au yanamchukiza?
Ni muhimu kwa kila Mwislamu inapofika jioni kuyahesabu na kuyatathmini matendo yake ya kutwa nzima na kujiangalia amefanya mangapi yanayompendeza Allah na mangapi yanayomchukiza Allah.
Ikiwa yanayomfurahisha Allah ni mengi kuliko yanayomchukiza, basi alhamdulillah kwa siku hiyo hatakuwa mwenye khasara kubwa hata hivyo itahitajika kwake alete istighfaar kwa yale makosa aliyoyafanya na kuweka azma ya kutorejea tena.
Ama ikiwa matendo yanayomchukiza Allah ni mengi kuliko yanayomfurahisha, basi hiyo itakuwa ni hasara kwake katika siku hiyo na atahitajika kuharakisha kuleta istighfaar na kumuomba Allah msamaha na pia kufanya mambo mema kwa wingi kwani wema hufuta uovu kama Allah anavyosema: “… Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka.” [Hud (11): 114].
Faida
Ndugu wa Kiislamu, kuanza kujihesabu mwenyewe kuna faida kubwa ambayo itamwezesha mtu kwa taufiq ya Allah kuweza kupata hesabu nyepesi siku ya Kiama.
Mwenye kuhesabiwa kwa hesabu nyepesi atakuwa ni mwenye kufuzu na mwenye furaha kama anavyoyaeleza hayo Allah kwa kusema: “Ama atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia. Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi. Na arudi kwa ahali zake na furaha.” [Al-Inshiqaq (84) : 7-9].
Kinyume cha mja kuanza kujihesabu mwenyewe kutampelekea kufanya mambo mengi maovu pasi na yeye kujali na hatimae kuingia katika kundi la watakaokuwa na hesabu nzito.
Kundi hili abadani halitapata maisha ya furaha huko akhera, bali watapata maisha ya tabu na adhabu nyingi (Allah asitujaalie kuwa katika kundi hili). Allah anasema: “Atakayepewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake basi huyo ataomba kuteketea; na ataingia motoni.” [Al-Inshiqaq (84): 10-12].
Ndugu wa Kiislamu, bila ya shaka tumeuona umuhimu wa kuanza kujihesabu mapema wenyewe kabla hatujahesabiwa na Allah ili kuepukana na adhabu za milele kwani atakayehesabiwa na Allah na akahukumiwa kuingia motoni hatakuwa na wa kumlaumu isipokuwa nafsi yake. Amesema Allah (subhanahu wata’ala) katika hadith Qudsiy:
“Enyi waja Wangu, ni vitendo vyenu Ninavyovihesabu, kwa ajili yenu Nikakulipeni. Kwa hivyo anayekuta wema amshukuru Allaah na yule anayekuta yasiokuwa mema (basi) ajilaumu mwenyewe.” [Muslim].
Tunamuomba Allah (subhanahu wata’ala) atuhesabu kwa hesabu nyepesi na atujaalie tuwe wenye kuzihesabu nafsi zetu kila tunapotaka kufanya jambo letu ili tuliwache endapo litamchukiza Allah (subhanahu wata’ala) na kuendelea nao ikiwa litamridhisha. Amin.