Wakazi wa Makongeni wafurahia kukarabatiwa kwa barabara ya BAT-Kiganjo
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Thika wamefurahia uzinduzi wa barabara ya BAT-Kiganjo ambayo imekarabatiwa kwa kiwango cha kisasa.
Barabara hiyo ilizinduliwa Alhamisi na Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina.
Alisema kilio cha wahudumu wa usafiri kimekwisha sasa baada ya barabara hiyo kuzinduliwa rasmi.
Alisema barabara hiyo ya BAT itakwenda hadi Kiganjo ambako kuna wakazi zaidi ya 70,000.
“Nina imani kubwa ya kwamba wafanyabiashara katika sekta zote watanufaika wote na hata ajali ndogondogo zilizoshuhudiwa kila mara zitapungua kwa asilimia kubwa,” alisema Bw Wainaina.
Alisema kuna barabara nyingine ya Kenyatta Highway-Pilot-Broadway-Umoja itakayounga kwa ile kuu ya Garissa.
Wahudumu wa matatu na bodaboda walishukuru serikali kwa kufanya hima kuona ya kwamba barabara hiyo imewekwa katika hali nzuri inayostahili.
Dereva aelezea furaha yake
Dereva wa matatu ya Thika-Makongeni, Bw Boniface Ngugi, alisema hiyo ilikuwa ni siku kubwa kwao kwani barabara hiyo itageuza shughuli zote za eneo hilo la Makongeni.
“Hapo awali barabara hiyo ilikuwa ndogo ambapo hata magari mawili kupishana ilikuwa ni shida, lakini sasa imekuwa pana ajabu ambapo sasa kutakuwa na usafiri wa kuridhisha kila dereva,” alisema Bw Ngugi.
Alisema mashimo mengi yaliyokuwa hapo awali yamekwisha na sasa magari yanasafiri bila matatizo.
“Lakini kile tungeomba ni tuwekewe matuta katika sehemu tofauti ili kuzuia ajali zinazoweza kutokea kila mara. Watoto wengi wa shule ya msingi na ya upili za Kenyatta huvuka barabara hiyo wakienda na kutoka shuleni,” alisema Bw Ngugi.
Naye Bw James Mburu ambaye ndiye mwenyekiti wa wahudumu wa bodaboda kituo cha Makongeni, alisema sasa biashara itanoga kwelikweli kwa sababu mashimo yaliyoshuhudiwa hapo awali hayatakuwepo tena.
“Tunaona kazi iliyofanywa hapa ni ya maana kweli kwa sababu wahudumu wa usafiri wataendesha kazi yao kwa njia nzuri bila kuhangaika. Tunashukuru jambo hilo,” alisema Bw Mburu.