Habari

Hisia mseto tarehe ya Gavana Waiguru kuolewa ikikaribia

June 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa Kaunti ya Kirinyaga, watumiaji wa mitandao ya kijamii pamoja na viongozi kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya wana hisia mseto baada ya Gavana wa Anne Mumbi Waiguru kuwaalika kwa harusi yake itakayofanyika Julai 13, 2019.

Ijumaa, mijadala mitaani ilikuwa ya ucheshi kuhusu hafla hiyo, vijana wakiwa na ule utundu wao wa kawaida, wazee wakiwa na ustaarabu wa kimaoni nao kina mama wakiungaNa pamoja kufurahia siku hii muhimu ya Gavana wa Kirinyaga.

Wenye kuegemea kwa siasa na hasa wanaomuunga mkono wamesisitiza kuwa harusi ni suala la kibinafsi la Waiguru.

Nao wanaompinga wamechukua fursa hiyo kurusha mishale ya kumpunguza makali.

Wengi wanasema kuwa hii ni hafla tu ya kawaida ambayo inahusu maisha ya kibinafsi ya Gavana wao, wengine wakisema wanatarajia kujitokeza kwa harusi hiyo kujivinjari mapochopocho huku wengine wakianza kuingiza siasa katika suala hilo.

Kuna mtumiaji wa mtandao wa Twitter anayejiita @BonnyK ambaye ameandika: “Sasa safari ya Waiguru ya kuelekea kuwania ugavana katika Kaunti nyingine ambayo ndiyo ya mumewe imeanza.”

Anaongeza: “Na ikiwa atawania ugavana wa Kirinyaga mwaka wa 2022, ina maana kuwa yeye ndiye amemuoa huyo mwanamume.”

Kwa mujibu wa msaidizi wa kisiasa wa Waiguru, ambaye ni diwani mstaafu Muriithi Kang’ara, “hii ni siku kubwa ya gavana wetu ambapo anakimbizana na utulivu wake wa kimaisha.”

Anasema kuwa maisha ya ndoa ya Waiguru hayako katika Katiba na hakuna yeyote anafaa kujadili suala hilo kwa msingi wa kisiasa.

“Kuna tofauti kubwa sana kati ya Gavana Waiguru na Waiguru kama mtu binafsi. Ako na maisha yake ya kindani na hayo hayako katika ukadiriaji wa kiutendakazi kama gavana,” amesema Bw Kang’ara.

Naye Askofu Karimi Kibuchwa wa Kanisa la Anglikana anasema Gavana aliyetulia katika moyo wake ni Gavana ambaye atakuwa na moyo uliotulia akihudumia wakazi.

“Gavana Waiguru kupata mtu wa kumuoa ni baraka kubwa katika maisha yake na pia ni kielelezo bora kwa wote ambao wangetaka kutangaza hadharani kuolewa kwao lakini wanasitasita pengine kwa kuogopa kuchambuliwa na umma,” amesema Askofu Kibuchwa ambaye anasisitiza pia kwamba ndoa sio uhaini.

Wakili

Katika uwanja wa Kiamugumo, Bi Waiguru atafunga pingu za maisha na mpenziwe Kamotho Waiganjo ambaye pia ndiye wakili wake.

Katika kesi iliyoandaliwa na Bi Martha Karua wa Narc Kenya akipinga ushindi wa Waiguru katika uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Waiganjo alichangia pakubwa ushindi wa Waiguru kudumishwa ambapo alimenyana kufa kupona na Wakili Gitobu Imanyara wa Bi Karua.

Itakumbukwa kwamba licha ya Karua kuwa mwanasiasa, ni wakili pia ambaye ashawahi kuhudumu kama hakimu hapa nchini na pia Waziri wa Masuala ya Kikatiba na Haki.

Ina maana kuwa Bw Waiganjo kumenyana na kesi hiyo haikuwa suala rahisi, na sasa baadhi watadhani kujituma kwake kulikuwa na msukumo wa kipekee ambapo alikuwa akinusuru sio tu mteja, bali jiko.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mbunge wa Starehe, Kasisi Margaret Wanjiru, Gavana Waiguru anafaa pongezi za dhati na watu wajitiokeze kwa wingi kuipamba kama mashahidi.

“Huu ni ujasiri mkuu na nafurahia sana hafla hii ya dadangu Waiguru,… Mungu aibariki ndoa yake na aidumishe na awape maharusi hawa wawili raha ya kimaisha iliyojaa ufanisi mkuu,” amesema Bi Wanjiru.

Anasema kuwa mijadala itakayozuka kuhusu harusi hii itakuwa ya kila aina, wengine walio na utundu wa kimaisha wakisema yao, walio wa nia njema wakisema yao na wasio na lao la kumakinikia wakiwa na yao ya kusema.

“Watu wanafaa waelewe kuwa wale ambao hawajawahi kuafikia mapenzi ya dhati huwa na kijiba na wale ambao wameyaafikia,” amesema Wanjiru.

Habari za ndoa yao zilianza kujitokeza kwa umma Februari 26, 2019, ambapo wawili hao waliandaa sherehe ya kitamaduni ya posa siku kadhaa baada ya Februari 16 ambapo Bw Kamotho alilipa mahari.

Wawili hao washawahi kuwa katika husiano zingine za kimapenzi uchumba na ndoa na kuzifutilia mbali ndio sasa wajiweke katika hafla hii wote wakiwa wamevuka mstari wa umri wa miaka 50.