Jaji aamua mzazi wa kiume pia anaweza kulea watoto akitengana na mke
Na PETER MBURU
JAJI Joel Ngugi ametoa uamuzi ambao huenda ukamaliza mgogoro wa miaka mingi baina ya wazazi wa kike na wa kiume, akisema hata baba anaweza kumlea mtoto sawa na mama, na kuharamisha dhana ya muda mrefu kuwa mama tu ndiye anafaa kupewa jukumu la kulea.
Jaji Ngugi wa Mahakama Kuu ya Nakuru alisema kuwa ni kupotoka kuamini kuwa wanaume hawawezi kulea, ila wanaweza kuwa wa kutafuta riziki tu.
Alitoa uamuzi huo katika kesi ambapo mzozo kuhusu mzazi aliyefaa kumlea mtoto, kati ya wanandoa waliokosana na kutengana ilifikishwa mbele yake, kufuatia kisa ambapo mwanamume alimfumania mkewe akifanya ngono na mfanyakazi wao wa nyumbani.
Mwanamume huyo alipoteza haki ya kulea wanawe wawili 2014, wakati mahakama ya chini iliamua kuwa hakuwa na haki ya kuwalea wanawe, kwa kuwa alifaa kuwa akitafutia familia riziki.
Hakimu katika kesi hiyo aliamua kuwa ilikuwa vyema kwa mkewe kuwalea watoto, badala ya kuishia kulelewa na wajakazi.
“Ingawa mlalamishi alihakikisha kuwa atawasimamia wajakazi moja kwa moja, naona kuwa hii haitadumu kwa muda kama mwanamume, mara kwa mara atahitajika kushughulika kazini na mwishowe ataachia wajakazi majukumu ya ulezi,” akasema hakimu huyo.
“Ikiwa naweza kuamua kwa kweli, ni vigumu kwa mwanamume kutekeleza majukumu ya ulezi,” Hakimu M Otindo akaamua.
Dhana
Lakini mwanamume huyo alikata rufaa katika Mahakama Kuu, ambapo Jaji Ngugi aliamua kuwa ni dhana mbaya kuamini kuwa wanaume wameumbwa kuwa watafuta riziki, nao wanawake kuwa walezi.
Alisema uamuzi wa mahakama ya chini unaweza kutoa ishara mbaya kuwa kina mama wazuri wanafaa kukaa nyumbani na wana wao, nao kina baba wazuri kuwa nje wakitafuta riziki.
“Kufikiria namna hii ni hatari na kunaweza kuleta tatizo. Kutegemea dhana zisizo za kweli kutoa uamuzi si haki kwa wahusika,” akasema Jaji Ngugi.
Jaji huyo alimkosoa hakimu kuwa alitegemea dhana na imani zisizofaa kutoa uamuzi.
Aliamua kuwa wazazi wote wana haki ya kushiriki katika ulezi wa watoto.
Ripoti ya maafisa wa watoto iliyofikishwa kortini ilisema kuwa watoto walipendelea kuishi na baba yao.