• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Mkuu wa mashtaka afutwa huku kesi ya Bashir ikianza

Mkuu wa mashtaka afutwa huku kesi ya Bashir ikianza

Na MASHIRIKA

KIONGOZI wa jeshi nchini Sudan, Alhamisi alimfuta kazi Mkuu wa Mashtaka wa nchi hiyo siku chache baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar Al-Bashir kushtakiwa kwa ufisadi na maandamano mapya kuanza.

Kufutwa kwa Al-Waleed Sayyed Ahmed, kulijiri wakati naibu wa Abdel Fattah al-Burhan katika baraza tawala la kijeshi, alitangaza kuwa aliyepanga uvamizi dhidi ya waandamanaji mnamo Juni 3 alitambuliwa.

Abdallah Ahmed atachukua nafasi ya Al-Waleed Sayyed Ahmed kama Mkuu wa Mashtaka, shirika la habari la Sudan, SUNA lilitangaza lakini halikutoa maelezo zaidi au sababu za kufutwa kwa Al- Waleed.

Mnamo Jumapili, Bashir alifika mbele ya mwendesha mashtaka mwingine kujibu mashtaka ya ufisadi na kupatikana na pesa za kigeni kinyume cha sheria.

Kufutwa kwa Al-Waleed kunajiri wiki kadhaa baada ya watu waliovalia mavazi ya kijeshi kushambulia waandamanaji nje ya makao makuu ya kijeshi.

Baraza tawala la kijeshi limekanusha kwamba liliagiza waandamanaji hao watawanywe na kusisitiza kuwa liliagiza msako katika eneo linalouzwa dawa za kulevya linalojulikana kama Colombia.

Baraza limesema kwamba msako huo ulitekelezwa baada ya mkutano na wakuu wa sheria na usalama ambao Al-Waleed Sayyed Ahmed alihudhuria.

Wiki jana, alieleza wanahabari kwamba alihudhuria mkutano huo lakini aliondoka kabla ya suala la operesheni hiyo kujadiliwa. “Nilipokuwa hapo, suala la kutawanya waandamanaji halikutajawa,” alisema.

Madaktari wanaoshirikiana na wanaopanga maandamano wanasema kwamba watu wapatao 128 wameuawa tangu msako ulipoanza, wengi wao wakati waandamanaji walitawanywa.

Vifo

Wizara ya Afya ilisema ni watu 61 waliuawa. Naibu wa mkuu wa baraza tawala la kijeshi Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, Alhamisi alisema kwamba aliyepanga uvamizi dhidi ya waandamanaji ametambuliwa.

Hata hivyo, alikataa kutaja jina la mshukiwa akisema hakuna haja ya kuvuruga uchunguzi.

“Hata akiwa ni nani, awe anatoka majeshi ya kawaida au raia, atashtakiwa. Uchunguzi utakuwa wa wazi na kesi itahudhuriwa na umma,” alisema.

Waandamanaji wanasema kwamba operesheni ilitekelezwa na wanachama wa kikosi hatari kinachosimamiwa na

Dagalo. Hata hivyo, alitetea kikosi chake akisema yeyote anaweza kununua sare za kikosi hicho kutoka sokoni na kuzivaa.

“Jana tulimkamata Jenerali mmoja kwa kusambaza vitambulisho vya kikosi hicho,” Dagalo alisema.

  • Tags

You can share this post!

Vizingiti vyaongezeka katika juhudi za kumshtaki wakili

MUTUA: Morsi hakuwa dikteta na kifo chake ni huzuni

adminleo