• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:25 PM
MWANAMUME KAMILI: Katika ulaji wa raha zenu msichafue bustani zetu

MWANAMUME KAMILI: Katika ulaji wa raha zenu msichafue bustani zetu

Na DKT CHARLES OBENE

BINADAMU anaweza kuwa jitu kwa vipawa alivyotunukiwa, lakini si kitu pasi na mazingiza mema.

Ulimwengu tunamoishi unapendeza kila kiumbe hata chukizi nzi mpenda harufu.

Nani asiyetaka hewa safi na upepo mwanana uvumao kutoka milima na vijilima?

Nani asiyependa maji safi kwenye mito na chemichemi inayolisha miti na wanyama wa pori?

Mabonde na tambarare ndimo tunamoishi sisi kina yakhe tunaobahatisha maisha.

Mbona tuuharibu wema wa mazingira kwa utupaji taka na mipira ya plastiki?

Jamani wanaume kwa wanawake, hii mipira ya kondomu iliyotapakaa katika nyanja wanamochezea watoto ilitoka wapi?

Kwa nini watu wazima kushindwa kutumia akili vyema?

Kati ya viumbe wote wanaoishi ulimwenguni, hakuna mmoja aliyepevuka akili zaidi ya binadamu na ambaye anatumainiwa kuendeleza wema, kuimarisha hali na hadhi ya ulimwengu.

Hata hivyo uharibifu unaotekelezwa na wanaume kwa wanawake unachusha.

Uharibifu huu wa ulimwengu ndio kwanza kipigo chake mja wa leo.

Tembelea maeneo wanamolala watu wazima kwa shughuli za kiutu uzima uondokewe na akili za kibinadamu.

Maeneo gani hayo? Vyumba vya kulala wasafiri pamoja na vyumba vya kulazwa wasafirishwao anga za mahabani si makazi yanayostahiki tena.

Uchafu kwenye majaa na uharibifu umetokana hasa na kuwepo mipira ya kondomu iliyotupwa kiholela ama iliyoachwa ovyo baada ya wenye vyao kuridhika na vitamu.

Ghadhabu zangu zinatokana na ukweli kwamba wanaotupa mipira hii si watoto wadogo wendao chekechea.

Ni watu wazima; wanawake kwa wanaume waliojaaliwa hekima na akili. Iweje basi watu wazima kushindwa kudumisha hadhi na kulinda hali ya mazingira?

Mbona watu wazima wakaamua kuzorotesha hewa ya mabustani na nyanja wanamochezea watoto? Nakumbuka nilivyopenda sana kucheza mwajificho vichakani enzi za utotoni.

Mtoto yupi wa karne hii anaweza kutia pua kwenye vichaka pasipo kuona haya?

Misitu ya kondomu

Jamani watu wazima tahadharini msije kuza misitu ya mipira ya kondomu.

Na wala msininukuu kivoloya! Sijawakataza kutumia mipira ama kula vyenu vichakani na madanguroni. Sina uwezo kuwanyima haki yenu. Katika ulaji wa raha, msijesahau kwamba mtu ni utu.

Walaji hawa wa vichakani wamo mbioni kukwamiza juhudi za kuboresha mazingira.

Utupaji mipira hii ni mojawapo ya sababu za kuchafuka mito na vijito sisemi kuzibwa kwa mitaro ya majitaka. Hata hivyo hilo si kubwa.

Mipira ya kondomu katika nyanja wanamochezea watoto ni hatari na tishio kubwa kwa hali na afya ya watoto hao. Hawa watoto wa masikini wamezoea kuokota na kupuliza hewa ndani mwa puto na vibofu. Ndio mchezo wa watoto waliolelewa katika uduni wa vinyago ama vifaa vya kuchezea watoto. Nani atawalaumu watoto hao kuokota mipira ya kondomu na kuchezea wanavyotaka?

Isitoshe, hawa watoto wa masikini wanaweza kuokota taka zote wakidhani ni puto. Angalau watazitundika nyumbani wakajikumbusha “Happy Birthday!” Hebu tafakari madhara ya watoto kuchezea hii mipira ya watu wazima. Hata mifugo kama mbuzi wako hatarini kutafuna nakshi zote kwenye mipira iliyotupwa kiholela. Jamani wanaume wa leo, mwatakaje kutukosesha utamu wa mbavu za mbuzi!

Hili jambo la watu kutapakaza mipira ya kondomu kwenye nyanja na nyasi wanamochezea watoto sharti lipewe uzito unaostahili. Hatuwezi kustahimili aibu wanayopata wazazi wanaoshangaa kuona wanao wakichezea ama wakisafisha mipira ya kondomu waliyookota uani. Watoto wadogo walijua wapi tofauti kati ya puto na mipira hii ya wakware wa mitaani?

Mwanamume kamili sharti kujua kwamba wajibu wa mtu mzima ni kufanya mambo yanayolingana na akili na umri wake. Kila mmoja wetu sharti kuwajibika kutunza mazingira tunamoishi kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo! Ni wakati wa kuchukua hatua kali zaidi ya maonyo kwa wakiukaji wanaochafua mabustani yetu. Huo ndio wajibu wa mwanamume kamili.

[email protected]

You can share this post!

Misri ya Mohamed Salah yaanza AFCON kwa ushindi japo...

Jubilee yamkana Khalwale

adminleo