• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
Kizaazaa pacha wakitibua jaribio la kuwatenganisha

Kizaazaa pacha wakitibua jaribio la kuwatenganisha

Na BENSON AMADALA

KULIZUKA kizaazaa eneo la Fufural, Likuyani katika Kaunti ya Kakamega, wasichana pacha walioungana majuzi walipotibua jaribio la kuwatenganisha na mwenzao aliyelelewa pamoja na mmoja wao.

Wasichana hao walikimbilia kituo cha polisi Alhamisi usiku kutafuta hifadhi, baada ya mtafaruku kuzuka baina ya familia mbili zinazohusika.

Iliripotiwa kuwa mzozo ulianza wakati Shem Abuti, jamaa wa familia ya pacha hao alipomwendea Bi Angelina Omina Omulama, mamake Melvis Imbayi na wakaanza kuzomeana.

Pacha hao, Sharon Mathius na Melon Lutenyo, pamoja na Melvis walikuwa wamewasili Kakamega kutoka Nairobi na walikuwa wakielekea kukutana na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya wakiwa na Bi Omulama.

Lakini inaripotiwa kuwa Bw Abuti alimwendea Bi Omulama na kuanza kumvuruga baada ya kutofautiana kuhusu binti yake Melvis Imbaya.

Bw Abuti alimlaumu Bi Omulama kwa kutaka kuondoka na binti yake, ambaye alikuwa ameeleza nia ya kuendelea kuishi na familia ya Sharon na Melon, katika kijiji cha Fufural, eneo la Likuyani.

Polisi walisema Bi Omulama alitumia bodaboda pamoja na binti yake na wakaondoka kuelekea mahali kusikojulikana wakati wa tukio hilo.

Sharon na Melon nao waliondoka na kutorokea kituo cha polisi cha Kakamega kuripoti kisa hicho na ikiwalazimu polisi kukimbia kusuluhisha suala hilo.

Baadaye, maafisa hao walimpata Bi Omulama pamoja na binti yake na wakawapeleka kwa maafisa wa kuwahudumia watoto, ambapo Sharon na Melon walikuwa wakati huo.

Kuheshimu uamuzi wa watoto

Baada ya kukutana na wazazi wa pande zote kwa muda, kamanda wa polisi wa kaunti hiyo Bernard Muli alisema kuwa familia hizo zilikubaliana kusuluhisha tofauti zao na wakaahidi kuheshimu uamuzi wa watoto hao wanaotaka kuendelea kuishi pamoja.

“Wasichana hao wameshtuka kutokana na kilichotokea na wanahitaji kurejea katika hali ya kawaida na kurudi shuleni kuendelea na masomo. Hawataki picha zao zitumiwe katika vyombo vya habari kwa kuwa wanatatizika,” alisema Bw Muli.

Bw Muli aliwataka wanahabari kutowapiga picha wasichana hao wala wazazi wao.

“Mambo haya yanawasababishia wasichana hao na familia zao mshtuko, tuheshimu uamuzi wao,” akasema Bw Muli.

Baba ya Melvis alisema baada ya mkutano, familia zote zilikubaliana kuwa watoto hao waendelee kuishi pamoja ili maisha yao yasitatizike.

“Tungependa kuwaona watoto wetu wakiishi pamoja na kuendelea na masomo yao bila kutatizika. Tunataka wawe pamoja kwa kuwa ndiyo mapenzi yao,” alisema Bw Lutah Maruti.

Matamshi yake yalikuwa sawa na ya baba wa pacha hao aliyesema kwamba waliamua kuheshimu uamuzi wao wa kuishi pamoja.

“Tunashauriana kuhusu njia bora zaidi ya kusuluhisha suala hili na mambo yanaendelea vyema,” alisema Bw Lukokha.

Alisema kanisa fulani limejitolea kugharamia elimu ya watoto hao hadi chuo kikuu. Wazazi hao walisema wanao watarejea shuleni Jumatatu.

Matokeo ya uchunguzi wa DNA kuhusu familia hizo yalitolewa Jumamosi iliyopita, yakionyesha kuwa Sharon Mathius na Melon Lutenyo ni pacha wa toka nitoke. Uchunguzi huo ulifanywa na shirika la Lancet Kenya. Ripoti hiyo ilionyesha kuwa Bi Onyango si mama ya Mevis Imbaya na kuwatambua wazazi wake kuwa Angeline Omina na Bw Wilson Lutah Maruti.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Ni chakula kipi bora kwa ng’ombe wa maziwa?

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Jinsi ya kushughulikia dosari za...

adminleo