Habari Mseto

Moi kuuza mifugo ya wenye kipato cha chini kujilipa gharama ya kesi

June 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SAM KIPLAGAT

RAIS Mstaafu Daniel Moi ameagiza madalali kuuza ng’ombe wa wafugaji kutoka Samburu waliomshtaki ili apate pesa alizotumia kugharimia kesi.

Mahakama iliagiza wafugaji hao kumlipa Mzee Moi Sh8.2 milioni aliposhinda kesi waliyomshtaki.

Kwenye barua kwa mawakili waliowakilisha wafugaji hao 249, wakili wa Moi Juma Kiplenge, alisema madalali ambao hakutaja majina yao kwa sababu za kiusalama watatwaa na kuuza mifugo hadi pesa zitakazopatikana zitoshe Sh8.2 milioni.

“Tumeagiza madalali wetu kukita kambi hadi shughuli hii itakapokamilika,” inasema barua kutoka wakili Kiplenge.

Wafugaji hao walipatiwa makataa ya kulipa ambayo tayari yamepita.

Walimshtaki Moi na Shirika la African Wildlife Fund katika mzozo wa shamba walilodai lilikuwa lao lakini wakashindwa kesi ilipoamuliwa 2017.

Wakiongozwa na Bw Joseph Lekamario, wafugaji hao walidai walikuwa wakimiliki shamba hilo la ekari 17,105, eneo la Laikipia Kaskazini.

Akitupilia mbali kesi hiyo, Jaji Lucy Waithaka alisema ushahidi ulionyesha kwamba hakuna wakati ambao jamii iliwapokonya wamiliki wa ardhi hiyo waliosajiliwa.

Ingawa walikata rufaa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Damacline Bosibori aliagiza jamii kulipa wakili wa Moi Sh8,267,666.

Bw Kiplenge, kupitia kampuni yake ya mawakili Kiplenge & Kurgat alikuwa akidai Sh40 milioni lakini msajili alipunguza hadi Sh8.2 milioni.

Wafugaji hao pia wanafaa kulipa kampuni ya mawakili ya Kaplan & Stratton, iliyowakilisha AWF katika kesi hiyo Sh11.8 milioni.