Wabunge vijana wanavyozembea mijadala muhimu bungeni
Na NYAMBEGA GISESA
WABUNGE vijana wameorodhoshwa miongoni mwa wasiochangia mijadala kwenye vikao vya bunge kwa miaka miwili iliyopita.
Mmoja wao ni mbunge mwenye umri mdogo zaidi, Bw John Paul Mwirigi wa Igembe Kusini.
Ripoti ambayo ilitolewa hivi majuzi kuhusu wabunge ambao hawachangii katika mijadala na hoja mbalimbali bungeni ilimuorodhesha kama mmoja wa wale ambao mchango wao katika mijadala ni duni mno.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Mzalendo Trust, amezungumza mara tano bungeni tangu Septemba 2017 hadi Desemba 2018.
Wabunge wengine ambao wako katika orodha ya wabunge kumi wazembe katika mijadala bungeni ni Alex Kosgey (Emgwen), Lilian Tomitom (Mbunge wa kaunti ya Pokot Magharibi) , Alfah Miruka (Bomachoge Chache), Sylvanus Maritim (Ainamoi), Anwar Loitiptip (Seneta wa Lamu), Kithua Nzambia (Kilome), Prengei Victor (seneta mteule mwakilishi wa vijana), Benjamin Mwangi (Embakasi ya kati) Jenerali wa Lang’ata’s Nixon Korir na mbunge wa Chepalungu Gideon Kimutai. Iwapo wabunge hao wamezungumza bungeni si zaidi ya mara kumi na tano.
Katika orodha ya wabunge ambao wamejitolea vilivyo kuchangia hoja mbalimbali bungeni, maseneta watatu walisifiwa kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, seneta wa Nairobi Johnstone Sakaja aliorodhesha kuwa katika mstari wa mbele akifuatwa na mwenzake wa Nandi Samson Cherargei huku seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot akifunga orodha ya wabunge watatu bora.
Katika bunge la kitaifa, mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro alitunukiwa nafasi ya kwanza kutokana na ukakamavu wake wa kuchangia kwa ufasaha hoja mbalimbali bungeni humo.
Katika nafasi ya pili ni Didmus Barasa (Kimilili), Kuria Kimani (Molo), Naisula Lesuuda (Samburu Magharibi), Silvanus Osoro( Mugirango Kusini) pamoja na Mwakilishi wa Wanawake kaunti ya Laikipia, Bi Catherine Waruguru alifunga orodha ya kumi bora.