JAMVI: Waiguru anavyopanga karata yake kwa 2022
Na BENSON MATHEKA
Kujitolea kwa Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru, kupatanisha makundi ya Tanga Tanga na Kieleweke katika eneo la Mlima Kenya kunaweza kuchukuliwa kama juhudi zake za kujiimarisha akilenga kuwa kigogo wa siasa eneo hilo, wadadisi wanasema.
Kulingana na baadhi ya wachanganuzi, juhudi za Bi Waiguru zinaweza pia kuwa na ‘baraka’ za Rais Uhuru Kenyatta ambaye inasemekana anamuamini sana licha ya kuzongwa na madai ya ufisadi alipokuwa waziri.
“Ni kibarua kigumu, iwe ni kwa hiari yake akilenga kutimiza malengo yake ya kibinafsi ya kisiasa au akiwa amekabidhiwa jukumu hilo na watu wengine, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta ambaye anataka kuona ngome yake ya kisiasa ikiwa imeungana,” asema Dkt Sammuel Waigwa, mchanganuzi wa siasa za Mlima Kenya.
Wiki jana katika mkutano wa vuguvugu la Embrace ambalo linashirikisha wabunge na wanasiasa wanawake wanaounga muafaka kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Bi Waiguru alisema yuko tayari kupatanisha viongozi wa eneo la Mlima Kenya ambao kwa wakati huu wanaonekana kugawanyika.
Kundi la Kieleweke linapinga azma ya Naibu Rais William Ruto ya kumrithi Rais Kenyatta nalo kundi la Tanga Tanga linasema eneo hili
linafaa kumrudishia mkono Dkt Ruto kwa kumuunga Rais Kenyatta tangu 2013.
Kulingana na kundi la Kieleweke linaloshirikisha mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu na mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda, Dkt Ruto amekuwa akikaidi Rais Kenyatta kwa kuendeleza siasa za mapema badala ya kuzingatia maendeleo.
Kundi hilo linadai kwamba Dkt Ruto hawezi kulinda na kutetea maslahi ya jamii za Mlima Kenya baada ya Rais Kenyatta kumaliza kipindi chake cha pili kwa sababu amekuwa akipinga vita dhidi ya ufisadi, na muafaka kati ya Rais na Bw Odinga.
Vilevile, linamlaumu Dkt Ruto kwa ufisadi, madai ambayo hakuna anayeweza kuthibitisha. Kundi hili lina ‘baraka’ za wazee wa jamii ya Agikuyu ambao wamekuwa wakisisitiza kuwa eneo la Mlima Kenya halina deni la kisiasa la kumlipa Dkt Ruto.
Nalo kundi la Tanga Tanga linasisitiza kuwa eneo hilo linafaa kumheshimu Dkt Ruto na kumuunga mkono ili kufuta nembo ya usaliti kwa kutounga viongozi wa makabila mengine kugombea urais. Miongoni mwa viongozi wa kundi hilo ni wabunge Kimani Ichung’wa, Ndindi Nyoro, Alice Wahome na Gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu.
Makundi hayo yamekuwa yakishambuliana vikali na hii ndiyo iliyomfanya Bi Waiguru kujitolea kuyaunganisha.
Kulingana na gavana huyo, viongozi wa kisiasa kutoka Mlima Kenya wanafaa kuungana na kuzika tofauti zao badala ya kugawanyika na kumlaumu Rais Kenyatta kwa kupuuza eneo lao.
“Tunataka kuungana kwanza kama wakazi wa Mlima Kenya. Na ikiwa wengine wameshindwa kuunganisha watu wetu, ninajitolea kutekeleza hilo. Tutaketi, tusikilize maoni yenu na kutafuta mwelekeo tutakaofuata katika miaka mitatu iliyobaki (kabla ya 2022),” alisema Bi Waiguru akiwa Murang’a.
Hata hivyo, wadadisi wanasema yeye si wa kwanza kusema atajaribu kupatanisha eneo hilo. Kulingana na Bw Francis Wangai, mchanganuzi wa siasa, kupatanisha mirengo ya Kieleweke na Tanga Tanga eneo la Mlima Kenya kwa wakati huu, kunahitaji kujitolea, mwongozo na mwelekeo kutoka kwa Rais Kenyatta.
“Ikiwa Waiguru ambaye inasemekana anamezewa mate na wagombeaji wa urais kuwa mgombea-mwenza 2022 ana baraka za Rais Kenyatta, anaweza kufaulu lakini ikiwa ni juhudi zake pekee anaweza kugonga mwamba.
“Hisia zangu ni kwamba ni Rais Kenyatta pekee anayeweza kumaliza siasa za mgongano zinazoshuhudiwa katika ngome yake, jambo ambalo linaonekana hayuko tayari kufanya kwa wakati huu,” anaeleza Bw Wangai. Anasema juhudi za Bi Waiguru, japo zinafaa, zinaweza kuchukuliwa na pande zote kama kutaka kujijenga kuwa msemaji wa eneo hilo.
“Kumbuka kwa sasa, Rais Kenyatta hajasema lolote kuhusu atakayechukua nafasi yake kama msemaji wa jamii na inachukuliwa kuwa kuna pengo la uongozi katika eneo la Mlima Kenya kwa sababu hajatoa mwelekeo kuhusu suala hilo. Kwa hivyo, inachukuliwa kila anayejaribu kujitolea kuunganisha makundi hayo anataka kujipigia debe kuchukua wadhifa huo,” aeleza Bw Wangai.
Bi Waiguru anakiri kwamba ni Rais Kenyatta tu anayepaswa kulipa eneo hilo mwelekeo wa kisiasa kuhusu mgombea urais anayefaa kuungwa mkono katika uchaguzi wa 2022. Anasema kuwa hakuna kiongozi mwingine anayeelewa matatizo ya wakazi wa Mlima Kenya kuliko Rais Kenyatta na kwa hivyo wanasiasa wanapaswa kusubiri mwelekeo wake.
“Na tukubaliane kama watu wa Mlima Kenya kuungana na kuzungumza kwa sauti moja. Tuna viongozi wa kutosha kutoka hapa kwetu na tunapokosea, tuelezeni lakini sio kubomoa nyumba yetu,” alieleza.
Wadadisi wanasema ni muda tu utakaoamua iwapo juhudi za Bi Waiguru zitafaulu kwa sababu pamekuwapo juhudi za kuunganisha jamii kupitia kongamano la tatu la Limuru ambazo hazijafaulu huku wahusika wakihisi kuwa ni mapema mno kuandaa mkutano huo.
Mnamo Mei mwaka huu, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi walisema kuna haja ya kongamano hilo kufanyika ili kuweka mikakati ya kuelekea uchaguzi wa 2022 na kuteua msemaji wa eneo la Mlima Kenya.