• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:55 AM
Maisha ya wanyama pazuri baada ya Ziwa Nakuru kusafishwa

Maisha ya wanyama pazuri baada ya Ziwa Nakuru kusafishwa

NA RICHARD MAOSI

Mbuga ya Ziwa Nakuru, sasa limesafishwa katika mojawapo ya juhudi za kukabiliana na maji taka yanayoingia mbugani.

Wasimamizi wa mbuga walitumia huduma za vijana wasiokuwa na ajira kutoka mitaa ya Bondeni, Kivumbini, Lake view Freearea na Flamingo kusafisha mito inayobeba uchafu huo.

Vibarua walizoa jumla ya tani 1.5, na baadaye tani 4.2 idadi inayofikisha zaidi ya tani 6.0 kwa siku mbili mfululizo.

Hili linaashiria jinsi kina cha uchafuzi wa mazingira kwenye ziwa Nakuru umeshamiri,na baadhi ya wafanyikazi wanaona litajwe kuwa janga la kitaifa linalokodolea macho mbuga nyingi humu nchini.

Shughuli hiyo ilivutia hisia mseto huku maswali mengi kuliko majibu yakiibuka, endapo KWS ina bajeti ya kung’arisha mbuga za wanyama.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, mwangalizi wa utalii kutoka kutoka mbuga ya wanyama ya Ziwa Nakuru Bw Sirman Kioko, alisema maji taka yamekuwa yakiingia kwenye mbuga kutokana na miundo msingi duni.

Aliongezea kuwa maisha ya wanyama hasa simba, nyati, vifaru,nchui,nviboko na flamingo yalikuwa hatarini,kwa sababu ya maji taka yalikuwa yamebadili mkondo na kupenyeza kwenye mbuga.

Miaka mitano iliyopita mbuga ya Nakuru ilikuwa na idadi kubwa ya ndege aina ya heroe ,lakini sasa wamebakia 200 tu.

Hali hii itazidi kuwa mbaya,endapo idara husika haitaweka mikakati ya kutafuta suluhu la kudumu kwa wanyama pori wanaozidi kuangamia.

Aidha uchafuzi katika ziwa Nakuru umefanya ndege kuhamia ziwa Bogoria ambapo inaaminika angalau chakula ni tele.

“Tunakubali kuwa gharama ya kusafisha mbuga ni kubwa,lakini pia tunaomba umma kupunguza matumizi ya mifuko ya plastiki inayoziba njia za maji,”alisema.

Pia aliongezea kuwa ni jukumu la mbuga kusafisha mazingira ya wanyama,lakini baraza la mji wa Nakuru pia lina nafasi kubwa ya kuhakikisha makazi ya watu ni safi,kwa kuzoa taka ipasavyo.

Anaona kuna utepetevu mkubwa kutoka kwa usimamizi wa mazingira NEMA,wanaostahili kuweka sheria kali za kukabiliana na wale wanaoharibu mazingira.

Aliongezea kuwa baraza la kusimamia huduma za wanyama pori (KWS),halina bajeti ya kusafisha mbuga na ndio sababu waliwaajiri vibarua saba kuendesha shughuli hiyo ya siku tatu.

Uchafuzi wa mito inayoingia ziwa Nakuru hutokea msimu wa mvua ambapo maji hufurika na kusomba taka kutoka kwenye makazi ya watu .

Wanyama wanaovutia watalii kama vile Nyati hupata maradhi pindi wanapokunywa maji chafu,yaliyochanganyika na mifuko ya plastiki.

Licha ya KWS kumiliki kituo cha kufanyia utafiti aina ya maradhi mbalimbali yanayokabili wanyama bado hawajafanikiwa kwa asilimia kubwa kuyazuia.

Hili linajiri siku moja tu baada ya wakazi wa mtaa wa Bondeni kuandamana barabarani wakilalamikia,ongezeko la kiwango cha takataka kwenye makazi ya watu.

You can share this post!

Umma waonywa dhidi ya kulipia kazi za sensa

KUPPET yamtetea mwalimu aliyedaiwa kutunga mimba mwanafunzi

adminleo