• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mke aruka buda katika kikao cha kugawa ardhi

Mke aruka buda katika kikao cha kugawa ardhi

Na CORNELIUS MUTISYA

MAMA wa hapa alidhihirisha ujasiri usio wa kawaida alipomruka mumewe katika kikao cha wazee wa ukoo waliokuwa wakitatua mzozo wa shamba baina ya mumewe na ndugu zake.

Kulingana na mdaku wetu, mume wa mama huyo ndiye aliyekuwa kifungua mimba katika familia ya watoto wanne, wanaume watatu na msichana mmoja. Baba yao aliaga dunia wakiwa wangali wachanga.

“Watoto hao waliachwa na baba yao mzazi wakiwa wangali wachanga. Walibaki mikononi mwa mama yao aliyehakikisha wamesoma hadi kidato cha nne,’’ alisema mdokezi.

Inasemekana kwamba, kifungua mimba wa familia hiyo alipohitimisha masomo yake ya sekondari, alioa na akajitoza katika kilimo cha mboga na matunda.
Jamaa huyo alinyakua shamba lote la familia. Ndugu zake waligeuka maskwota katika ardhi ya wazazi wao.

Hata hivyo, hakuna masika yasiyo na mbu, ndugu zake walichanuka na wakaamua kushinikiza kupewa mgao wao kama watoto wa boma hilo. Vurugu zilizuka mpaka wazee wa ukoo wakaingilia kati ili kusuluhisha utata huo.

“Wazee wa ukoo waliandaa kikao cha dharura ili kutuliza rabsha iliyokuwa imezuka katika familia hiyo,’’ alisema mdaku wetu.

Yasemekana kwamba, mke wa kifungua mimba alinyanyuka na akawaambia wazee kuwa alikuwa akifadhaishwa moyoni na mienendo ya mumewe ya kuwanyima ndugu zake kipande cha shamba walime ilhali walikuwa watoto wa familia moja!

“Mume wangu ni mdhalimu kupindukia. Ametwaa shamba lote la familia na kuwanyima ndugu zake hawa mgao wao. Ananikera mno,’’ mama watoto alipasua mbarika.

Duru zaarifu kwamba, matamshi ya mama huyo yaliwafurahisha wazee hao mpaka wakaamua kuwagawia ndugu hao haki yao.

You can share this post!

Yabainika viwanja viwili vya ndege havina hati

Kocha wa Vihiga awatia nari vijana wake kudhidhirisha...

adminleo