• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
WAKILISHA: Mfano bora kwa wenzake mtaani

WAKILISHA: Mfano bora kwa wenzake mtaani

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA umri mdogo wa miaka 15, yuko mbioni kuhakikisha kwamba anaorodheshwa miongoni mwa marapa wa kike wanaotamba sio tu humu nchini, bali ulimwenguni kote.

Hii ni ndoto yake Beatrice Mwikali Mueni al-maarufu Cate Ilah, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, shule ya upili ya Dandora Girls, mtaani Dandora.

Kufikia sasa ametunga nyimbo nne za injili na kilimwengu, lakini kutokana na changamoto ya ukosefu wa fedha, bado hajafanikiwa kuingia studioni.

Kinachofanya hadithi yake kusisimua ni kwamba yeye mwenyewe ndiye anajiandikia kazi zake huku akipata chocheo kutokana na masuala ya kawaida katika jamii.

“Aidha, utunzi wangu hasa ni kwa minajili ya kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu muziki wa rap, na kudhihirishia jamii kwamba hiki kitakuwa kivukio cha kunifanikisha maishani,” asema.

Mbali na kuwa anatumai kwamba utunzi huu utamsaidia kujikwamua kutoka maisha ya umaskini, pia unamsaidia kupata kitulizo kutokana na maisha magumu na uovu unaohusishwa na vitongoji duni.

“Idadi kubwa ya wakazi wa mtaa huu ni maskini kumaanisha kwamba ni rahisi kwa vijana kujihusisha na matumizi ya mihadarati, wizi au ukahaba. Muziki huu umeniepusha na haya yote kwani natumia muda wangu mwingi kutunga ngoma badala ya kufuatana na magenge,” aeleza.

Kutokana na hili, familia yake na hasa mamake amekuwa shabiki wake sugu na licha ya kutokuwa na uwezo wa kifedha kumsaidia kutimiza ndoto yake, amekuwa akiunga mkono jitihada zake.

Ni ukakamavu huu ambao majuma kadha yaliyopita ulimsaidia kuwa mmoja wa vijana waliopata ufadhili kutoka kwa Franky’s Entertainment, kampuni ambayo imeibuka kusaidia wasanii hasa kutoka vitongoji duni.

“Majuma machache yaliyopita, nilisikia habari kwamba shirika hili lilikuwa linatafuta vipaji mtaani. Nilienda kujaribu bahati yangu na nikafanikiwa. Tayari nishafanya shoo yangu ya kwanza Juni 15, ambapo nilipata fursa ya kutumbuiza mbele ya wasanii chipukizi kama mimi. Aidha, shirika hili linajadili mkataba wa kunisaidia kusajiliwa kama msanii, mbali na kuahidi kunitafutia shoo siku za wikendi,” aeleza.

Cate Ilah alizaliwa eneo la Bondeni, katika kitongoji duni cha Mathare ambapo kipaji chake cha uimbaji kilijitokeza akiwa katika darasa la sita.

Akosa karo ya kutosha

Alifanya mtihani wake wa darasa la nane mwaka 2018 na kupata alama 300 ambapo alipaswa kujiunga na shule ya Kalawa Girls High School, lakini kutokana na ukosefu wa karo, hakuweza kufanya hivyo.

“Mamangu hangeweza kumudu kunilipia karo, vile vile kushughulikia ndugu zangu wawili. Hili lilinivunja moyo sana na kunifanya kuhisi kana kwamba sintaweza kuendelea na masomo,” asema.

Lakini hakufa moyo kwani mapema mwaka huu alifanikiwa kupata ufadhili kutoka kwa serikali na kujiunga na kidato cha kwanza katika Dandora Girls Secondary.

Huenda ukadhani kwamba haiwezekani kwa mwanafunzi huyu kumakinika kimasomo na wakati huo huo kufanikisha ndoto yake kama mwanamuziki hasa wa rap, lakini kwa msichana huyu, nidhamu ya kufuata ratiba yake vikali imemwezesha kusawazisha yote mawili.

Kwa sasa anafanya kila awezalo kuimarisha kipaji chake.

“Nimewekeza mawazo yangu hapa kwani nina imani kwamba nitaweza kupenya,” aeleza.

Anawashauri vijana wenzake wasife moyo licha ya changamoto maishani. “Licha ya magumu unayopitia maishani, usijiruhusu kupoteza matumaini. Tumia kipaji alichokupa Mungu na utaenda mbali,” aongeza msichana huyu ambaye amekuwa kigezo cha wenzake mtaani.

You can share this post!

Puuzeni madai ya mpango wa kumuua Ruto – Wabunge

MAPOZI: Cedo

adminleo