• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Rotich apewa siku 10 kujibu kesi ya bima ya bodaboda

Rotich apewa siku 10 kujibu kesi ya bima ya bodaboda

Na RICHARD MUNGUTI

WAZIRI wa Fedha Henry Rotich na Mwanasheria Mkuu wamepewa siku 10 kujibu kesi waliyoshtakiwa na Gavana Mike Sonko akipinga mpango wa kuwashurutisha wanaoendesha bodaboda na tuktuk waanze kuzilipia bima.

Jaji Weldon Korir aliyeratibisha kuwa ya dharura kesi hiyo iliyowasilishwa na Gavana Mike Sonko, Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria, waliokuwa wabunge Kalembe Ndile na Reuben Ndolo na mwanasiasa Stanley Livondo aliwaamuru washtakiwa Rotich na AG (Jaji Paul Kihara Kariuki) wawasilishe majibu katika muda wa siku 10.

“Kesi hii inazua masuala mazito ya kisheria na kikatiba,” alisema Jaji Korir.

Bw Kalwa alimweleza Jaji Korir kuwa washtakiwa hawajawasilisha ushahidi mahakamani licha ya kukabidhiwa nakala za kesi hiyo wiki iliyopita.

Kesi hiyo ilipowasilishwa kortini Ijumaa , Jaji Onesmus Makau aliamuru washtakiwa wawasilishe majibu kufikia Jumatatu (jana) kuhusu madai ya walalamishi kwamba haki zao na hali zao za kiuchumi zitaathirika iwapo watalipa ada ya bima.

Bw Kalwa alimweleza Jaji Korir,“Bw Rotich na AG hawakuwashirikisha umma kabla ya kupeleka mapendekezo hayo bungeni.”

Wakili wa Serikali aliomba muda kuwasilisha majibu.

Akitoa uamuzi Jaji Korir alisema, “Washtakiwa wamepewa siku kuwasilisha majibu katika kesi hii ya Gavana Sonko na wengine inayozua masuala mazito kikatiba na kisheria kuhusu ukandamizwaji wa haki za wanaoendeleza biashara ya boda boda na Tuk-Tuk. Kesi itasikizwa Julai 25.”

Bw Rotich alisema katika makadirio ya bajeti wanaoendesha boda boda na Tuktuk watahitajika kulipa bima kugharamia wateja wao na wanaotembea kwa miguu endapo ajali itatokea.

Gavana Sonko anasema kuwa wanaoendesha biashara hii hawakushirikishwa kabla ya Bw Rotich kupeleka mapendekezo hayo katika bunge.

You can share this post!

AFCON: Kivumbi chatarajiwa kwa ‘fainali ndogo’...

Kenya yaridhika na nishani ya fedha magongo ya barafu

adminleo