Kenya yaridhika na nishani ya fedha magongo ya barafu
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya Kenya ya mpira wa magongo ya barafu (Ice Hockey), Ice Lions, iliridhika na nishani ya fedha katika mashindano ya Madaraka Day Cup yaliyoandaliwa katika hoteli ya Panari jijini Nairobi.
Ikiongozwa na nahodha Ben Azegere, Ice Lions iliandikisha matokeo mseto katika awamu ya mechi za mzunguko kabla ya kampeni yake ya kuvizia taji kuzimwa na Marekani kwa kuchapwa 10-9 kwenye fainali iliyoamuliwa katika muda wa ziada. Timu hizi zilikuwa zimetoka 9-9 katika muda wa kawaida.
Kenya, ambayo inanolewa na kocha Robert Ouko Opiyo, ilianza mashindano kwa kupoteza 17-13 dhidi ya Team Europe. Hata hivyo, ilijinyanyua na kushangaza Marekani 13-6 katika mechi ya pili na kutinga fainali kwa kucharaza Canada 6-4.
Baada ya siku mbili za mashindano, Ouko alisema Ice Lions ilifurahia matokeo yake. “Timu ilijaribu sana. Tulijiandaa vyema. Ingawa tulipoteza dhidi ya Marekani katika fainali, tunafurahia matokeo yetu ambayo pia yalijumuisha kuchapa Canada katika awamu ya kwanza.”
Wafungaji wa Kenya katika fainali walikuwa Gedion Amiani (mabao matatu), Peter ‘Pinches’ Mburu (mawili), Arnold Mburu (penalti), Video Omwenga (mawili) na Benjamin Njoroge (bao moja).
Canada iliridhika na medali ya shaba baada ya kuaibisha Team Europe 13-1.
Matokeo: Juni 22 – Mechi ya kwanza: Kenya 13-17 Europe, Mechi ya pili: Canada 6-9 Marekani, Mechi ya tatu: Europe 17-11 Canada, Mechi ya nne: Kenya 13-6 Marekani, Mechi ya tano: Kenya 6-4 Canada; Juni 23 – Mechi ya kutafuta mshindi wa nishani ya shaba: Canada 13-1 Europe (wachezaji wengi hawakufika uwanjani), Fainali: Kenya 9-10 Marekani.