Mali yaponda Mauritania, Angola wakiyumbisha dau la Tunisia
Na MASHIRIKA
CAIRO, MISRI
MALI walifungua kampeni za Kundi E kwa matao ya juu zaidi kwa kuwaponda limbukeni Mauritania 4-1 mnao Jumatatu usiku katika mchuano ambao umezalisha mabao mengi zaidi hadi kufikia sasa kwenye fainali za AFCON.
Ushindi huo unaning’iniza padogo matumaini ya Tunisia ambao kwa sasa wana ulazima wa kuwakomoa Mali katika mchuano wao wa pili mnamo Ijumaa.
Tunisia ‘The Carthage Eagles’, waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Angola ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Mauritania mnamo Jumamosi.
Abdoulay Diaby aliwaweka Mali kifua mbele kunako dakika ya 37 kabla ya Moussa Marega kufunga mkwaju wa penalti mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kufanya mambo kuwa 2-0.
Mabao mengine ya Mali yalifumwa wavunia kupitia kwa Adama Traore wa AS Monaco na somo wake Adama Traore wa Metz, Ufaransa katika dakika za 55 na 73 mtawalia.
Mauritania ambao wanashiriki fainali za AFCON kwa mara ya kwanza katika historia, walifutiwa machozi na Moctar Sidi El Hacen kupitia penalti dakika ya 72.
Djalma Campos, 32, alifuta jitihada za Youssef Msakni mwishoni mwa kipindi cha pili na kuwapa Angola alama moja muhimu katika sare ya 1-1 waliyoisajili dhidi ya Tunisia.
Campos ambaye kwa sasa ni fowadi wa Alanyaspor nchini Uturuki, alivurumisha kombora langoni pa Tunisia baada ya kipa Farouk Mustapha kushindwa kuudaka mpira alioelekezewa na Mateus Galiano.
Msakni alikuwa amewaweka Tunisia kifua mbele kunako dakika ya 34 kupitia mkwaju wa penalti.
Licha ya kuwa kikosi nambari mbili barani Afrika kwa mujibu wa viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Tunisia walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara huku Angola ambao wakitamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha pili.
Uongozini
Nusura Angola almaarufu ‘Palancas Negras’ walijipate uongozini kunako dakika ya 22, Wilson Eduardo akapaisha mpira safi aliopokezwa na Stelvio Rosa da Cruz.
Bao la Tunisia ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Alain Giresse, lilikuwa zao la masihara ya beki Manuel ‘Paizo’ Troco aliyemchezea Naim Sliti visivyo ndani ya kisanduku.
Kipa Tony Cabaca wa Angola alilazimika kufanya kazi nyingi za ziada mwishoni mwa kipindi cha pili huku akizipangua fataki za Msakni na fowadi wa zamani wa Sunderland, Wabhi Kazhri.
Tunisia kwa sasa wanajiandaa kwa kibarua kigumu dhidi ya Mali mnamo Ijumaa huku Angola ambao kwa sasa wana hamasa zaidi, wakishuka dimbani kupepetana na Mauritania siku moja baadaye.