Habari MsetoSiasa

Bunge la Kenya limejaa watoto, asema Munya kuhusu madai ya kuua Ruto

June 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

WAZIRI wa Biashara Peter Munya ameendelea kujitetea pamoja na mawaziri wenzake wanaodaiwa kupanga mpango wa kuua Naibu Rais William Ruto, akiyataja kuwa siasa.

Waziri huyo amesema walikuwa wakifanya kazi waliyopewa na Rais, na kuongeza kuwa hakuona umuhimu wa kumfahamisha Dkt Ruto kuhusu mikutano yao, kwa kuwa hatoki Mlima Kenya.

“Nilipopewa hiyo kazi na Rais, sikuona umuhimu wa kumfahamisha Dkt Ruto kuhusu mikutano hiyo. Yalikuwa masuala mahususi yaliyoibuliwa na watu wa kutoka eneo fulani, ambapo hatoki. Nilifaa kumwambia nini?” Bw Munya akasema alipokuwa katika mahojiano katika runinga moja humu nchini Jumanne usiku.

Lakini alisema haukuwa mpango wa kumficha ukweli, wala mikutano yenyewe haikuwa ya siri, akisema “angejua mwenyewe na aniulize ningemwambia.”

Waziri huyo alisema halikuwa jukumu lake kuzunguka akitangazia watu kuwa walikuwa wakikutana.

“Huwa watu wanakutana, nazungumza hata na mawaziri wenzangu tunapopatana, lakini kwani ni lazima niende kwa naibu rais kumwambia nimekutana na waziri fulani?”

Aidha, waziri huyo aliwakashifu wabunge kwa majibizano wanayoendeleza kuhusu madai hayo, akisema wana utoto.

“Tunafaa kuwa wakomavu, siasa za kenya ziko na utoto mwingi sana na watoto wamejaa hilo bunge,” akasema Bw Munya.