• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Tangatanga wataka Munya na wenzake wajiuzulu

Tangatanga wataka Munya na wenzake wajiuzulu

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE saba kutoka mrengo vuguvugu la ‘Tangatanga’ sasa wanawataka mawaziri wanaodaiwa kupanga njama ya kumuua Naibu Rais William Ruto wajiuzulu wakisema wameiharibia serikali sifa kwa kujiingiza katika “uhalifu”.

Wakiongozwa na mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, wabunge hao Jumatano walisema kwa hatua ya mawaziri hao kufanya mikutano ya kisiri waliodai ni ya maendeleo katika hoteli za binafsi ni ukiukaji wa hitaji la Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili ya maafisa wa umma.

“Tunamtaka Waziri wa Biashara Peter Munya na wenzake kujiuzulu kwa kushiriki njama zao za uhalifu. Ni maendeleo gani walikuwa wakijadili usiku katika hoteli ya kibinafsi ilihali kuna afisi za serikali ambako mikutano kama hiyo inaweza kujadiliwa?” akauliza Bw Baraza kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Mbunge huyo alisema ni makosa kwa mawaziri hao kutoka Mlima Kenya kukutana katika hoteli kujadili maendeleo ya eneo hilo ilhali waliteuliwa kuhudumia taifa lote kwa jumla.

“Swali ni je, nani watajadili maendeleo kutoka maeneo mengine ya nje ambako hamna mtu aliyeteuliwa katika baraza la mawaziri?” akauliza Bw Barasa.

Aliandamana na wenzake, Mbw Vincent Musyoka (Mwala), Mathias Robi (Kuria Mashariki), Mohamed Ali (Nyali), Stanley Muthama (Lamu Magharibi), kati ya wengine wanaotoka maeneo ya nchi ambako hakuna aliyehudumu kama waziri katika serikali ya sasa.

Bw Ali alidai kuwa njama ya kumzima Naibu Rais zilianza miezi kadha katika kaunti ya Lamu wakati ambapo Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini Francis Atwoli alidai kuwa jina la Naibu Rais halitakuwa kwenye karatasi za kupigia kura mnamo 2022.

“Baadaye alinyimwa maafisa wa usalama katika mikutano yake Nyeri na maeneo mengine nchini. Tunataka kuwaambia kwamba wasijaribu kumuua mtu kwa sababu ya mamlaka yaliyo mikononi mwa raia,” akasema Bw Ali.

Naye Bw Musyoka alipuuzilia mbali madai ya Bw Munya kwamba walikutana kujadili maendeleo akihoji sababu ya kuachwa nje kwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ambaye pia anatoka eneo hilo la Mlima Kenya.

“Wizara ya Kilimo inayosimamiwa na Bw Kiunjuri ni muhimu zaidi katika Agenda Nne Kuu ya maendeleo ya serikali ya Jubilee. Mbona waziri huyu hakushirikishwa katika mikutano ya akina Munya katika mkahawa wa La Mada? ” akauliza Bw Musyoka.

“Hii ndio maana tunashuku walikuwa wakipanga uhalifu na wanafaa kujiuzulu haraka ili wajiunga na makundi kama vile Mungiki, Musumbiji na MRC,” akaeleza.

Mnamo Jumatano Bw Munya pamoja na wenzake Joe Mucheru (ICT) na Bi Sicily Kariuki waliitwa katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusiana na madai kuwa walipanga njama ya kumwangamiza Dkt Ruto.

Inadaiwa kuwa watatu hao waliitwa baada ya Naibu Rais kumpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa DCI George Kinoti kwamba watatu hao walikuwa wanapanga njama za kumuua.

Lakini akiongea na wanahabari baada ya kuhojiwa kwa saa mbili na maafisa wa DCI, Bw Munya alikana madai hayo akisema hayakuwa na ukweli wowote.

Hata hivyo, akikubali kwamba wamekuwa wakikutana katika mkahawa wa La Mada ulioko kando ya barabara kuu ya Thika, kujadili maendeleo ya eneo la Mlima Kenya.

You can share this post!

Kuria ashangaa kwa nini Matiang’i hajakamatwa kwa...

Mbunge mmoja TZ naye kapendekeza hatua kali dhidi ya Wakenya

adminleo