• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
Nipe nafasi niwanie urais 2022, Oparanya amwambia Raila

Nipe nafasi niwanie urais 2022, Oparanya amwambia Raila

Na PETER MBURU

GAVANA wa Kakamega Wycliffe Oparanya sasa anasema eneo la magharibi limechoka kuwa chini ya kivuli cha kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, akiamini pia naye ametosha mboga kuwa debeni katika uchaguzi wa 2022.

Gavana huyo alisema baadhi ya viongozi wamekuwa na hulka ya kuelekeza wakazi wa magharibi jinsi wanavyotaka, lakini akasema sasa viongozi wa eneo hilo wana usemi wa kutosha na hawatakubali tena.

“Tumesema wakati huu hakuna haja ya kuja hapa kusema watu wa Kakamega twende upande huu ama ule, hapana. Wewe kuja utafute viongozi wa eneo hili, tuketi utuambie mambo yako kisha uondoke urudi kwenu,” akasema Bw Oparanya.

Alimtaka Bw Odinga kumuachia fursa ya kutafuta kiti sasa, akisema ametosha.

“Sasa wewe baba ukizaa mtoto na amefika mahali anataka kupewa boma lake, si mpaka nipewe boma langu? Nitaendelea kuwa nawe kila siku? Nikitafuta boma langu ni mbaya kweli?” Gavana Oparanya akauliza.

Kundi la wabunge waliokuwa wameandamana naye wakiwemo wa Navakholo Emmanuel Wangwe, Tindi Mwale wa Butere na wengine aidha walimpigia debe gavana huyo, wakisema anatosha kuwania Urais.

“Sisi ambao tunafanya kazi nawe tunajua kuwa unaelewa kazi. Sina tashwishi kwamba gavana akipewa kiti chochote, akienda juu 2022 ama akitaka Urais ni mtu ambaye anaweza kufanya kazi,” akasema Bw Mwale.

Wabunge hao walilaumu mirengo ambayo eneo lao limekuwa likiunga mkono kuwa wanapowaunga mkono huwa wanapotea baadaye.

You can share this post!

Chepkoech na Manangoi wathibitisha kushiriki mbio za...

Asimulia mahakama daktari alivyobeba moyo na figo ya maiti

adminleo