Habari Mseto

Kobia aachiliwa kwa dhamana, wafanyakazi waachiliwa bila masharti

June 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA Paul Kobia aliyefikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na kashfa ya Sh170 milioni ya dhahabu aliachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 na wafanyakazi wake 13 wakaachiliwa huru bila masharti.

Hakimu mkazi mahakama ya Milimani Bi Sinkiyiani Tobiko alisema hakuna sababu zilizowasilishwa na mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji kuwezesha mahakama kuwazuilia washukiwa hao kwa siku 14.

Bi Tobiko alisema lazima DPP awasilishe ushahidi kuthibitisha kuna ushahidi wa kutosha katika madai yanayowasilishwa mahakamani.

“ Hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa kuwezesha hii mahakama kumsukuma ndani Kobia pamoja na washukiwa hawa wengine 14,” alisema Bi Tobiko.

Wakili Henry Kurauka alipinga vikali ombi la DPP la kumsukuma Kobia ndani akisema kifungu nambari 49 (1) (h) cha katiba kinaitaka mahakama kuachilia mshukiwa hata uchunguzi ukiendelea.

Bi Tobiko alimwachilia mshukiwa huyo kwa dhamana ya Sh100, 000 pesa tasilimu na kuamuru kesi hiyo itajwe Julai 12 DPP aeleze ikiwa amewafungulia washukiwa mashtaka.

Kobia alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kileleshwa baada ya kuhojiwa kwa masaa matano..

Afisi ya mkurugenzi wa jinai DCI ilisema mshukiwa alitiwa nguvuni baada ya ripoti alikuwa amemtapeli raia wa Dubai $1.7milioni.

Kobia alitiwa nguvuni pamoja na Simeon Wanaina, Paul Gichuhi, Benjamin Mutisya, Patrick Mweu, Samson Kibet, Faith Kioko, Joyce Wenani, Miriam Nyambura, Consolata Thirindi, James Masai, Doreen Kathambi, Tanya Yvonne Goes na Gabriel Ndururi Murage.

“Baada ya uchunguzi fito za dhahabu , magari sita ya kifahari, stempu ya benki kuu ya kenya –CBK-, mashine ya kuhesabu pesa, mashine ya ETR na stempu kadhaa mbali mashine nyingine za kuunda dhahabu,” maafisa wa DCI walisema.

Akizugumza na wanahabari kabla ya kusukumwa kizuizini Kobia alisema kutiwa nguvuni kwake ni njia ya kumzuia asiwanie urais mwaka wa 2022.