Makala

Bwanyenye wa kigeni anavyowatesa wakazi wa Nakuru

June 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

RICHARD MAOSI, PHYLLIS MUSASIA NA KEVIN ROTICH

Wakazi wa Kiamunyi katika Kaunti ya Nakuru wameendelea kukadiria hasara kubwa baada ya maeneo hayo kukumbwa na mafuriko kufuatia mvua inayoendelea kunyesha.

Mvua iliyoanza kunyesha mwendo wa saa kumi na moja jioni siku ya Jumatano, ilisababisha mafuriko ndani ya nyumba za wakazi na zile za biashara.

Shughuli nyingi zilikwama baada ya maji kujaa ndani ya nyumba hizo huku nguo, malazi na mali ikilowa maji.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo Dijitali walisema mafuriko hayo yamesababishwa na ukosefu wa mitaro maalumu ya maji huku wngine wakikashifu mradi wa kilimo unaoendeshwa na raia mmoja wa kigeni kwa jina Madrugada Garden kwa kutumia njia mbovu ya unyunyuzaji maji mimea bila kuzingitia mbinu kamili inayohitajika.

Wakazi wahangaishwa na mafuriko Kiamunyi, Nakuru. Picha/ Phyllis Musasia

“Licha ya maeneo haya kukosa mitaro ya kupitisha maji ya mvua, kunaye bwanyenye mmoja wa kigeni ambaye anaishi upande wa juu wa sehemu hii. Anafanya kilimo lakini mbinu anayotumia si kamilifu,” akaeleza Bi Grace Mwanda mmoja wa wakazi wa Kiamunyi.

Mkazi mwingine Jeremy Lang’at alisema maji hayo ni hatari sana kwa afya ya wakazi haswa watoto ambao mara nyingi hulazima kulala kwenye nyumba zilizojaa maji na baridi kali.

“Tumezidi kusikitika jinsi hali hii imeendelea kwa muda sasa bila serikali ya kaunti kufanya lolote. Ni wajimu wa viongozi tuliowachagua kuhakikisha kuwa hali afya zetu pamoja na usalama kwa jumla unatiliwa maanani,” akasema Bw Langa’t.

Hili ndilo shamba la mwekezaji wa kigeni linaloelekeza maji katika makazi ya watu. Picha/ Richard Maosi

Ongezeko la mvua kubwa katika kaunti ya Nakuru pia imesababisha maeneo ya mabanda kwenye sehemu ya chini ya Nakuru Magharibi kama vile Kaptembwa, Kwa Ronda, Ponda Mali na sehemu zingine kushuhudia mafuriko.

Mchanga, mawe na mimea imesombwa na kutapakaa kila mahali huku baadhi ya barabara kuu zinazoelekea katika maskani ya watu zikiwa hazipitiki.

“Magari yaliyojaribu kupita yalikwama siku ya Jumanne, isipokuwa machache tu yaliyomudu kupata njia mbadala kuelekea mjini Nakuru,” alisema mzee wa mtaa Paul Ongeri.

Bw Ongeri alisikitika kuwa ukuta wa nyumba yake ulikuwa umebomolewa na mafuriko, alikuwa ameajiri vibarua wamsaidie kuchimba mitaro karibu na nyumba yake itakayosaidia kuelekeza maji.

Hii ni sehemu ya barabara iliyokatika ambapo wakazi wamehama huku wanafunzi wakitaabika. Picha/ Richard Maosi

Mkazo mwingine, Bi Ann Wangare alisema kuwa mwekezaji huyo wa kigeni anamiliki shamba la ngano na amekuwa akichangia matatizo ya wakazi wengi hapa. Alichimba mitaro katika shamba lake iliyoelekeza maji katika makazi ya watu.

Ingawa baadhi yao wamekuwa wakilalamika,hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na serikali ya kaunti ya Nakuru, huku idara husika ikionekana kufumbia macho swala hilo.

Hapo Jumatano asubuhi, wasimamizi wa Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu (KENHA) ,walifika katika eneo la tukio kutathmini kiwango cha uharibifu na wakaahidi kurejea tena lakini hadi wakati wa tukio hakuna aliyekuwa Nyanjani.

Baadhi ya wakazi walilazimika kukesha nje usiku wa kuamkia siku ya Jumatano kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha. Picha/Richard Maosi

“Wakazi wengi wanahofu kuwa athari inaweza kuwa mbaya zaidi hasa wakati huu ambapo,kiwango cha mvua ni kubwa,” akasema Ann.

Wiki tatu zilizopita wakazi wa Kiamunyi waliandamana barabarani kushinikiza serikali imchukulie hatua kali mwekezaji huyo wa kibinafsi, lakini wakatawanywa na polisi kupitia vitoa machozi.

Barabara za maeneo ya Kiamunyi zilivyoharibiwa na mafuriko. Picha/ Phyllis Musasia

Ann alieleza kuwa mwekezaji huyo amekuwa akiwahangaisha sio tu kwa kuyafungulia maji, bali pia kuwasha moto katika shamba lake msimu wa kiangazi.

Anasema moto huo umekuwa ukinea na kuvuka mipaka na wakati mwingine kuteketeza mali yao na mifugo.