Yafichuka Jaguar alitozwa Sh40,000 kwa mauaji
Na RICHARD MUNGUTI
MBUNGE wa Starehe Charles Kanyi Njagua, almaarufu Jaguar alitozwa faini ya Sh40,000 kwa kosa la mauaji mapema mwaka huu, mahakama ilifichuliwa Alhamisi.
Alipofikishwa kortini Milimani, Nairobi kwa madai ya kuchochea umma dhidi ya raia wa kigeni, upande wa mashtaka ulifichua uamuzi huo ambao uliwekwa siri tangu ulipotolewa Februari 2019.
Kiongozi wa Mashtaka, Bw Duncan Ondimu alitoa maelezo hayo kama mojawapo ya sababu ambazo aliamini Bw Njagua anastahili kuendelea kuwa kizuizini kwa siku 14 hadi uchunguzi kuhusu kesi yake ya uchochezi ukamilike.
“Mnamo Machi 21, 2017, mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama ya Baricho kwa makosa mawili ya kusababisha vifo kwa kuendesha gari vibaya na mnamo Februari 21, 2019, akahukumiwa na kutozwa faini ya Sh20,000 kwa kila kosa la sivyo kufungwa gerezani miezi sita na zaidi ya hayo akapigwa marufuku kuendesha gari kwa mwaka mmoja,” akasema Bw Ondimu.
Alipatikana na hatia ya kusababisha vifo vya mwendeshaji pikipiki Mugo Mwangi na abiria wake Joseph Maingi Kairia kwa kuendesha gari kwa mwendo wa kasi na kiholela.
Mbunge huyo atajua hatima yake Ijumaa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani Bi Sinkiyian Tobiko baada ya kuzuiliwa saa 24 kutokana na matamshi ya uchochezi yanayodaiwa yamevuruga uhusiano wa kibalozi kati ya Kenya na mataifa ya kigeni.
Bi Tobiko aliamuru mbunge huyo azuiliwe katika kituo cha Polisi cha Kileleshwa Nairobi anapoandaa uamuzi.
Hakimu aliamuru Bw Njagua asalie ndani kwa vile alikuwa na kazi nyingi ikiwemo kesi ya mfanyabiashara Paul Kobia aliyefikishwa kortini kwa kashfa ya dhahabu.
Bw Ondimu alisema mamlaka ya mawasiliano yameandikia baadhi ya vyombo vya habari kupata video inayomnukuu Njagua akitamka maneno hayo yaliyohujumu uhusiano wa kibalozi wa Kenya na mataifa ya kigeni.
Alisema mbunge huyo atawavuruga mashahidi akiachiliwa kisha akamsihi hakimu aamuru Bw Njagua azuiliwe uchunguzi ukiendelea.
Bw Ondimu alisema matamshi ya mwanasiasa huyo yamehatarisha usalama wa Wakenya wanaoishi nchi za kigeni.