MakalaSiasa

WANDERI: Madai ya njama ya kuua Ruto yasitiwe mzaha

June 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MADAI ya mauaji dhidi ya Naibu Rais William Ruto hayapaswi kuchukuliwa kwa urahisi. Hii ni kwa kuwa Kenya ina historia ya mauaji tata dhidi ya viongozi, ambapo ukweli wake umebaki kuwa siri hadi sasa.

Alipotoa madai kuhusu mikutano ya siri inayoendeshwa na baadhi ya viongozi wa ukanda wa Mlima Kenya kwa njama ya kummaliza, wengi walionekana kutochukulia kwa uzito kauli ya Dkt Ruto.

Kulingana naye, mikutano hiyo inaendeshwa kisiri na lengo lake kuu ni ‘kumzima kisiasa’ kutokana na azma yake ya kuwania urais mnamo 2022.

Ni wazi kuwa Kenya iko katika njiapanda kisiasa. Malumbano ya urithi wa Rais Uhuru Kenyatta yanafanana miaka miwili ama mitatu kabla ya 1978, wakati viongozi kadhaa wenye ushawishi kutoka jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA) waliungana kuhakikisha kuwa Rais Mstaafu Daniel Moi hangemrithi Mzee Jomo Kenyatta kama rais.

Wanasiasa hao walibuni kundi liitwalo ‘Change the Constitutional Movement’ (Vuvuvugu la Kubadilisha Katiba) ambapo lengo lake kuu lilikuwa kuona kuwa Bw Moi (ambaye alikuwa makamu wa rais) hakuchukua nafasi ya Kaimu Rais baada ya kifo cha Mzee Jomo Kenyatta.

Kulingana walioshuhudia harakati hizo, miongoni mwa njama hizo zilikuwa ni “kumnyamazisha” Bw Moi, hilo likimaanisha kumuua.

Mpango huo ulikuwa mkubwa kiasi kwamba, wanasiasa hao wanadaiwa kubuni “jeshi maalum” ambalo lingeshiriki katika njama hizo.

Simulizi kama hizo ndizo zinaandama vifo vya wanasiasa Tom Mboya, Josiah Mwangi Kariuki (JM) na Dkt Robert Ouko, ambaye alikuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni mnamo 1990.

Muda mfupi kabla ya kifo chake mnamo 1969, njama za mauaji ya Mboya zinadaiwa kupangwa vizuri na maadhi ya maafisa wenye ushawishi katika serikali ya Mzee Kenyatta.

Kulingana na ushahidi uliotolewa na Bw Nahashon Njenga, aliyefungwa gerezani kwa madai ya kuhusika na mauaji hayo, njama hiyo ilihusisha watu waliomwona Mboya kama ‘tishio la kisiasa’ kwa umaarufu wa Mzee Kenyatta.

Katika njama ya JM mnamo 1975, aliripotiwa kutoweka siku chache kabla ya mwili wake kupatikana umetupwa na kumwagiwa asidi katika msitu wa Ngong. Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa Dkt Ouko, ambapo mwili wake ulipatikana umetupwa katika mlima wa Got Alila mnamo 1990.

Hivyo, wakati Dkt Ruto anapotoa madai kuhusu maisha yake, ni suala linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito na asasi zote za usalama.

Hata hivyo, uchunguzi vile vile hauapaswi kuendeshwa kwa njia ya kuwapaka tope viongozi, hasa wale wametajwa. Kando na hayo, hii haipaswi kuwa njama ya kuzua taharuki ya kisiasa isiyofaa.

Ni wakati mwafaka kwa viongozi kufahamu kuwa urithi wa Rais Kenyatta haupaswi kugeuzwa njama ya kuifanya nchi mateka wa kisiasa.