Habari Mseto

Wakazi wa Juja wataka barabara eneo la Riuriro ikarabatiwe

June 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Riuriro, Juja waliandamana kulalamikia barabara mbovu eneo hilo.

Wakazi hao waliokuwa na ghadhabu walidai ya kwamba kwa zaidi ya miezi sita mfululizo, wameteseka pakubwa hasa wahudumu wa bodaboda na wafanyabiashara.

Bw Joseph Maina, mhudumu wa bodaboda alisema Jumatano wamepata shida tele kutokana na barabara mbovu katika kijiji cha Riuriro eneo la Juja.

“Wakati mwingi sisi hupata shida sana kunaponyesha kwani pikipiki zetu zinapata shida ya vipuri huku tukilazimika kuvibadilisha kila mara,” alisema Bw Maina.

Baadhi ya wahudumu wa bodaboda wakiandamana. Picha/ Lawrence Ongaro

Polisi waliofika eneo hilo walilazimika kukabiliana na wakazi wa eneo hilo kwani walidai kuwa ilikuwa haki yao kujengewa barabara.

Ilichukua muda wa saa tatu kabla ya maandamano hayo kukomeshwa na polisi, kwani waliwatawanya wakazi hao.

Wafanyabiashara pia hawakuachwa nyuma kulalamika wakidai kuwa hata kusafirisha bidhaa zao ni shida kubwa kwa sababu wanatozwa pesa mara dufu na wenye magari.

“Mimi hulazimika kulipa pesa nyingi ninapobebewa mizigo yangu hadi kwangu. Tunaiomba serikali kupitia mbunge wetu Francis ‘Wakape’ Waititu, kuingilia kati kuona ya kwamba wanakarabati barabara hiyo,” alisema Peter Mwangi ambaye ni mfanyabiashara eneo la Kenyatta Road, Juja.

Hali mbovu

Bw Godfrey Mucheke, ambaye ni diwani (MCA) wa wadi ya Kalimoni, alisema barabara hiyo ya kilomita moja iko katika hali mbovu ajabu.

“Ninatoa mwito kwa mbunge wa Juja Bw Francis ‘Wakape’ Waititu, ashirikiane na serikali ili kukarabati barabara hiyo inayopitia nje ya afisi kuu ya chifu wa Juja,” alisema Bw Mucheke.

Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba katika muda wa mwezi moja kuna jambo linalofanywa akishirikiana na mbunge huyo.

Hata hivyo, baada ya diwani huyo kuwahutubia wakazi hao walikubali kusitisha maandamano hayo huku wakitoa onyo kali kuwa iwapo hatua yoyote ya maana haitachukuliwa watarejea kwenye maandamano mara moja.