Habari Mseto

Passaris ajishindia kiti UN

June 29th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Nairobi, Bi Esther Passaris aliteuliwa Ijumaa mwanachama wa kamati moja katika Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Makazi, UN-Habitat.

Mbunge huyo sasa atakuwa mwanachama mpya wa kitengo cha Kisiasa cha Shirika la Afrika kuhusu Usalama Mijini (AFUS).

Kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa mojawapo ya mitandao ya kijamii, Passaris alisema kuteuliwa kwake kutachangia pakubwa katika ufanikishaji wa kazi ya UN-Habitat ya kuimarisha usalama mijini.

“Ni heshima kuu kwangu kuteuliwa kama mwanachama wa kamati tekelezi ya kitengo cha kisiasa cha shirika la African Forum on Urban Safety- AFUS. Nitajizatiti kuwezesha shirika hili kufikia lengo lake. Twende kazi, SDG Goal 5,” akasema Passaris.

Aliongeza kuwa atatumia cheo hicho kuimarisha mikakati ya kuzuia na kudhibiti visa vya uhalifu.

“Vijana, akina mama na wazee ndio waathiriwa wakubwa wa visa vya uhalifu katika mitaa na miji,” akaongeza.

Picha ya pamoja ikionyesha Esther Passaris. Picha/ Hisani