Habari Mseto

Kamket apuuza madai ya njama ya kumuua Ruto

June 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

MBUNGE wa Tiaty, William Kamket amepuuzilia mbali madai kwamba kuna njama ya kumuua Naibu Rais William Ruto.

Bw Kamket amesema kuwa madai hayo hayana msingi wowote, huku kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi akitaka naibu huyo wa Rais achukuliwe hatua za kisheria ikiwa madai hayo yatabainika kuwa uongo.

Bw Kamket alitaja madai hayo kama mbinu chafu zinazotumiwa na Dkt Ruto, na wafuasi wake, kujifaidi kisiasa baada ya kung’amua kuwa ushawishi wake unadidimia katika ngome zake.

Akiongea Ijumaa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Churo, iliyoko eneobunge lake, alipoikabidhi basi jipya, Bw Kamket alimtaka Naibu Rais akome kutumia propaganda ili Wakenya waweze kumhurumia.

“Ni kweli kwamba amepoteza ushawishi. Hii ndio maana ameanza kutumia propaganda na hadaa kwamba watu fulani wanapanga njama za kumwangamiza. Nani huyu anataka kummaliza? Huu ni mzaha wa mwaka,” alisema Kamket.

Mbunge huyo, ambaye ni mwandani wa Seneta wa Baringo Gideon Moi, alisema jamii ya Wakalenjin itaunga mkono azma ya seneta huyo ya kuwania urais mnamo 2022 na akamtaka Dkt Ruto kuwa tayari kwa wakati mgumu kisiasa kuanzia sasa.

“Umaarufu wa Gideon umeanza kuwatia baridi baadhi ya wanasiasa ilhali hajaanza kampeni. Hii ndio maana baadhi yao wameanza kuhadaa kwamba kuna njama ya kuwaua ili waweze kufufua umaarufu wao unaodidimia,” aliongeza Bw Kamket.

Mbunge huyo wa KANU alisema wafuasi wa Dkt Ruto wameanza kuingiwa na wasiwasi baada ya viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya kutangaza kuwa hawana deni la kisiasa za mtu yeyote na kwamba watampigia kura mgombeaji urais ambaye wanahisi kuwa atatetea na kuendeleza maslahi yao.

Bw Kamket alikariri kuwa KANU itadhamini mgombeaji urais katika uchaguzi mkuu wa 2022, na ambaye si mwingine ila Seneta Moi.

Machafuko

Kwa upande wake, Bw Mudavadi alisema Jumamosi madai ya Dkt Ruto kwamba kuna njama ya kumuua yanaweza kutumbukiza taifa hili katika machafuko.

“Madai kama haya yanapasa kuchunguzwa ili yasilete ghasia nchini. Ni ikiwa uchunguzi utabaini kuwa hayana msingi basi Naibu Rais anafaa kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa kutishia usalama wa nchi,” akasema Jumamosi katika Kanisa la Anglikana la St Thomas Cathedral, Kaunti ya Kirinyaga.

Naye Mbunge wa Mbeere Kaskazini, Bw Charles Muriuki Njagagua alisema usalama wa Dkt Ruto unafaa kuimarishwa zaidi na aombewe kufuatia madai kuwa kuna mipango ya kumuangamiza.

Alisema hayo katika Kanisa la Anglikana la Bishop Hanington, Mumias, Kaunti ya Kakamega wakati wa hafla ya kutoa shukrani iliyohudhuriwa na Dkt Ruto.

Barua moja, iliyosambazwa mitandaoni, yenye madai kuhusu njama ya kumuua Dkt Ruto inasema kuwa mkutano wa kupanga njama hizo ulifanyika katika mkahawa wa La Mada.

Mkutano huo ulidaiwa kupangwa na mawaziri wanne kutoka eneo la Mlima Kenya kuweka mikakati ya maendeleo katika eneo hilo.

Mnamo Jumatatu iliyopita mawaziri Peter Munya (Biashara), Joe Mucheru (ICT) na Sicily Kariuki waliamriwa kufika katika makao makuu ya DCI kuandikisha taarifa kuhusu suala hilo kwa msingi kuwa walikuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo wa La Mada.

Watatu hao hata hivyo, walikana madai ya kupanga njama hizo chafu.

Taarifa ya Florah Koech, George Munene  na Shaaban Makokha