HabariSiasa

Uhuru amzima Ruto

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ANITA CHEPKOECH

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali wito wa naibu wake William Ruto wa kufanyika kwa mkutano wa chama cha Jubilee.

Kupitia kwa msemaji wake, Bi Kanze Dena, Rais Kenyatta Jumanne alisema wito huo hauna umuhimu wowote kwani ni wa kisiasa.

Rais Kenyatta alitoa kauli hiyo akimjibu Dkt Ruto, ambaye mnamo Jumapili alisema angependa mkutano wa Jubilee ufanyike hivi karibuni ili kujadili masuala muhimu ya chama hicho.

Akizungumza katika Kanisa la St Luke’s PCEA katika eneobunge la Embakasi Mashariki jijini Nairobi, Dkt Ruto alisema mkutano huo utasaidia kufufua lengo la chama, kuleta umoja na mabadiliko Kenya, kutekeleza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni na kukita mizizi yake zaidi kitaifa.

Naibu Rais alieleza kuwa mkutano pia utawakumbusha viongozi wa Jubilee kuwa ni lazima wafanye kazi kwa umoja.

“Chama chetu ni cha kidemokrasia. Kwa hivyo ni sharti tujiandae kwa siasa za kitaifa kwa kuzingatia masuala, mipango na sera za kitaifa,” akasema Dkt Ruto.

Ili kusisitiza kuhusu umuhimu wa Jubilee kuandaa mkutano, Naibu Rais alitoa mfano wa vyama vya upinzani, ambavyo viongozi wao wamekuwa wakikutana, cha majuzi zaidi kikiwa ODM wiki iliyopita.

Awali, wito huo ulikuwa ukitolewa na wanasiasa wa kundi la ‘Tangatanga’ lakini Rais hakuwahi kuwajibu hadi wakati huu Dkt Ruto ametoa kauli yake.

“Suala kuhusu mkutano wa Jubilee ni la kisiasa. Sawa na jinsi bosi wangu amekuwa akisema, hatutajishughulisha na masuala ya kisiasa. Kama chama kitaitisha mkutano, basi ni sawa mkutano utafanyika,” akasema Bi Dena, kwenye kikao cha wanahabari.

Wanasiasa kwenye mrengo wa ‘Tangatanga’ wanaounga mkono azimio la Dkt Ruto kuwania urais 2022, wamekuwa wakimtia presha Rais Kenyatta aitishe mkutano wa Jubilee ili kujadili changamoto zinazotishia kukiporomosha chama hicho tawala.

Miongoni mwa wale ambao hulalamikia jinsi Rais, aliye kiongozi wa chama chao amekaa kimya licha ya misukosuko inayokumba Jubilee ni Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen, Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, mwenzake wa Nandi Samson Cherargei, na Mbunge wa Belgut Nelson Koech.

Viongozi hao wamekuwa wakitaka ajenda ya mkutano huo iwe ufafanuzi kuhusu lengo halisi la handisheki ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, na mwelekeo ambao chama kitachukua katika ugombeaji urais 2022.

Kutokana na jinsi wanavyoshuku handisheki inalenga kumharibia Dkt Ruto nafasi ya kushinda urais kwenye uchaguzi ujao, wafuasi wa ‘Tangatanga’ wamekuwa wakimtaka Rais Kenyatta atangaze wazi atamuunga mkono naibu wake.

Wito wa ‘Tangatanga’ kutaka mkutano wa Jubilee ulizidi baada ya Rais Kenyatta kuwakemea vikali kwa kueneza siasa badala ya kutumikia wananchi.

Bi Dena jana alisema Ikulu haitajadili madai ya njama ya kumuua Dkt Ruto.