Afisi ya Ouko yashutumiwa kuendeleza ukabila
Na Peter Mburu
WABUNGE wamelaumu afisi ya Mkaguzi Mkuu wa matumizi ya pesa za serikali kutokana na mfumo wake wa kuajiri wafanyakazi, wakisema haujakuwa na usawa wa kikabila.
Wabunge wa Kamati ya Maridhiano ya kitaifa na Usawa walisema orodha ya wafanyakazi katika afisi ya Dkt Edward Ouko wametoka jamii chache, na kuwa haisawiri utaifa.
Walidai kuna uwezekano kuwa shughuli za uajiri katika afisi hiyo hazina uwazi, na wakataka ripoti kuhusu maafisa ambao walitumika kuwahoji wafanyakazi wa ngazi za juu, katika afisi hiyo.
Wabunge hao walitilia shaka idadi kubwa ya wafanyakazi kutoka jamii fulani, huku zingine ama zikikosa uwakilishi au kuwa na watu wachache mno.
Kulingana na ripoti kutoka afisi ya Dkt Ouko kuhusu wafanyakazi, jamii zenye uwakilishi mkubwa ni Kikuyu (446), Luo (419), Kamba (150) na Luhya (146). Hii ni kati ya wafanyakazi wote 1607.
“Afisi hii imetoa mfano mbaya zaidi kati ya mashirika ya serikali, ilhali ndiyo inafaa kutoa mwelekeo kwa taifa. Itatubidi kumwita Dkt Ouko kufafanua kuhusu mfumo huu mbaya wa uajiri katika kikao kijacho,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Maina Kamanda (mbunge maalum).