Haji akejeliwa kutoshtaki wanyakuzi Mau
Na GEORGE SAYAGIE
BAADHI ya viongozi na wanaharakati wa kuhifadhi mazingira kutoka Kaunti ya Narok wamemlaumu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kwa kujivuta kuwakamata na kuwashtaki watu walionyakua ardhi msitu wa Maasai Mau.
Viongozi hao wanahisi kwamba, awamu ya pili ya kuwatimua maskwota hao haitakuwa na maana yoyote iwapo wale walionyakua ardhi hiyo hawatashtakiwa.
Mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel ole Kenta, alimlaumu Bw Haji kwa kulemaza juhudi za kukomboa msitu wa Mau ambao umezua mzozo kati ya jamii mbili.
“Tumeona Bw Haji akiwakamata watu ambao wametenda makosa ya uhalifu wa kiuchumi lakini kuharibiwa kwa msitu wa Mau ni mbaya kuliko uhalifu wa kiuchumi. Kujivuta kwa DPP kuwakamata watu hawa kunaibua maswali,” alisema Bw Kenta.
Bw Kenta alisema tayari polisi wamefanya kazi yao kwa kuwasilisha faili za watu hao kwa DPP na akashangaa kwa nini hawajakamatwa zaidi ya miezi kumi baada ya kuandikisha taarifa katika afisi za upelelezi wa jinai Kaunti ya Narok.
Kulingana na mshirikishi wa eneo la Rift Valley Bw George Natembea, zaidi ya vyeti 40 vya kumiliki ardhi katika msitu wa Mau vimerudishwa ili kufutiliwa mbali.
“Vyeti hivyo vilirudishwa kwa hiari na baadhi ya watu mashuhuri mwishoni mwa mwaka jana. Polisi pia wameandikisha taarifa kutoka kwa watu 15 waliohusika na ardhi ya msitu na faili ziko kwa DPP ili achukue hatua,” alisema Bw Natembeya.
Maafisa wa upelelezi wanachunguza mashamba makubwa yaliyo kwenye ardhi ya msitu kinyume cha sheria.
Wanachama wa mashamba ya Sisian, Reiya, Enoosokon, Nkaroni na Enakishomi wanapigwa darubini na wapelelezi ili waeleze walivyopata ardhi ya msitu kinyume cha sheria.
Ripoti ya jopo lililochunguza hali ya msitu wa Mau mnamo 2009 inasema kwamba, mashamba hayo matano yamo katika ardhi ya msitu wa Mau.
Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko, alipozuru Narok mwaka jana, alifichua kuwa vyeti 461 kati ya 716 vya kumiliki ardhi vilikuwa halali.
Bw Kenta ambaye amekuwa mmoja wa viongozi wanaotetea msitu wa Mau alitaja agizo la kutimuliwa kwa maskwota kama hatua muhimu katika kusimamisha kuharibiwa kwa msitu huo kulikofanyika kwa miaka mingi.
Malalamiko yake yanajiri huku Shirika la Huduma ya Misitu Kenya (KFS) likipiga marufuku wafugaji wanaolisha mifugo kwenye msitu huo.
Mkuu wa shirika hilo eneo hilo Mwai Muraguri alipiga marufuku shughuli za ufugaji katika misitu ya Mau, Olposimoru na Nyakweri msimu huu wa mvua.
Bw Muraguri alisema zaidi ya hekari 12,000 zimekombolewa tangu serikali ilipopiga marufuku ukataji wa miti katika msitu wa Mau.
“Hapa Narok, tuna asilimia 16.7 ya ardhi iliyo na misitu ikiwa ni zaidi ya asilimia 10 inayotakiwa kote nchini. Tunalenga asilimia 20 kufikia 2020 na ulishaji wa mifugo ndio tishi katika kutimiza lengo hili na ndio sababu tumepiga marufuku mifugo katika misitu hii,” alisema.