Makala

GWIJI WA WIKI: Paul Nganga Mutua

July 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

NIDHAMU ni kitu muhimu cha kudumishwa katika chochote unachokifanya.

Waheshimu watu na uishi nao vizuri.

Kila binadamu ana kipaji ambacho ni wajibu wake kukitambua na kutia azma ya kukipalilia.

Huwezi kabisa kujiendeleza maishani iwapo hujiamini. Kupiga hatua katika taaluma yoyote kunahitaji mtu kujibidiisha. Mwandishi mzuri lazima awe msomaji mzuri. Uvumilivu ni sifa nyingine muhimu na ya lazima kwa mtu kuwa nayo ili afanikiwe katika kazi ngumu ya uandishi.

Hatua ya kwanza katika safari yoyote ya ufanisi ni kufahamu kile unachokitaka; kujielewa wewe ni nani na kutambua mahali unakokwenda.

Usilie wala kukata tamaa usipofaulu. Pania kutenda mema ili umpendeze Mungu Muumba wako. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta.

Huu ndio ushauri wa Bw Paul Nganga Mutua – mwandishi wa Fasihi na mhariri ambaye pia ni mwalimu wa Kiswahili na Kiingereza katika Shule ya Upili ya Covenant Treasures, Nairobi.

Maisha ya awali

Nganga alizaliwa mnamo 1985 katika kijiji cha Kaumoni, Kaunti ya Makueni akiwa mtoto wa kwanza kati ya watano katika familia ya Bi Josephine Nduku na Bw Benedict Mutua Nganga.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Kaumoni HGM mnamo 1991 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Kaunguni iliyoko katika eneo la Makindu, Kaunti ya Makueni.

Alisomea huko kati ya 1992 na 1997 kisha akajiunga na Shule ya Msingi ya Wiivia, Makindu, mnamo 1998. Alama nzuri alizozipata katika mtihani wa KCPE mwishoni mwa 1999 zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya Starehe Boys’ Centre, Nairobi, mnamo 2000.

Alifanya mtihani wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2003 na kupata Gredi ya B iliyomkosesha fursa ya kujiunga na chuo kikuu kwa udhamini wa serikali.

Baada ya kusomea katika chuo anuwai cha Starehe Boys’ Centre mnamo 2004, alirejea sekondari akiwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Upili ya Ngara Queens, Nairobi. Aliufanya tena mtihani wa KCSE mwishoni mwa 2005 na akafaulu kupata Gredi ya B+.

Mnamo 2006, Nganga alianza kufundisha Kiswahili na somo la Bayolojia katika iliyokuwa Shule ya Upili ya Gurec, Nairobi (kwa sasa inaitwa Covenant Treasures School). Shule hii inapatikana katika mtaa wa Ziwani, eneo la Kariokor.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi mnamo 2007 kusomea Isimu na Fasihi ya Kiingereza japo matamanio yake makubwa yalikuwa ni kuzamia masuala ya ualimu au uanahabari.

Nganga anakiri kwamba mapenzi yake ya dhati kwa Kiswahili ni zao la kutangamana kwa karibu sana na baadhi ya walimu ambao walimpokeza malezi bora zaidi ya kiakademia.

Mbali na Bi Mwalyo na Bi Kilonga waliomtandikia zulia zuri la Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Wiivia, walimu wengine waliomshajiisha mno, kumtia katika mkondo wa nidhamu kali na kumhimiza pakubwa kutia bidii masomoni Bi Elizabeth Pamba wa Starehe Boys’ Centre na Bw John Mwaura ambaye kwa sasa hufundisha Kiswahili na somo la Historia katika Shule ya Upili ya Starehe Girls’ Centre, Kiambu.

Nganga anatambua pia ukubwa na upekee wa mchango wa marehemu Bw Yusuf King’ala ambaye hadi kufariki kwake mnamo 2005, alikuwa mwandishi msifika wa Isimu na Fasihi, mwalimu wa Kiswahili na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya kiakademia shuleni Starehe Boys’ Centre.

Zaidi ya kuchochewa kukichapukia Kiswahili darasani, Nganga anakiri kwamba mtagusano wake na Bw King’ala ulimwezesha kutambua kuwa lugha hii ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi.

Mchango kitaaluma

Akiwa mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza katika Chuo Kikuu cha Moi, Nganga alisomea kozi zote za Digrii ya B.A Kiswahili.

Hatua hiyo ilimkutanisha na Profesa Nathan Oyori Ogechi, Dkt Collins Kenga Mumbo, Dkt Mark Mosol Kandagor na Bw John Munyua ambao walipanda ndani yake mbegu zilizootesha ari zaidi ya kukipenda Kiswahili alaa kulihali.

Mnamo 2007, Nganga alichaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Kiswahili cha Moi (CHAKIMO) ambacho baadaye kilimwaminia nyadhifa za Naibu Mwenyekiti, Mhariri Mkuu na Mwenyekiti katika vipindi mbalimbali kati ya 2008 na 2011.

Zaidi ya kuchangia makala na habari mbalimbali kupitia kitengo cha ‘Nyundo Bin Twanga’ katika jarida la ‘Dafina Wiki Hii’ ambalo ni chapisho maalumu la CHAKIMO, Nganga alichangia makuzi ya Kiswahili chuoni Moi kwa njia tofauti.

Alianzisha kipindi ‘Dafina ya Lugha’ katika Idhaa ya MU-FM kila wiki na kwa mwaka mzima akawa kinara wa kipindi ‘Wajibu Wangu’ kilichopania kuwahamasisha Wakenya kuhusu nafasi yao katika utekelezaji wa Katiba Mpya ya Kenya mnamo 2010.

Zaidi ya kuwa mmoja wa watangazaji wa habari wa MU-FM, Nganga alishirikiana na wanafunzi wenzake kuchapisha ‘Mwongozo wa Utengano’ na pia kuigiza tamthilia ya ‘Kifo Kisimani’ iliyowahi kutahiniwa katika mitihani ya KCSE.

Isitoshe, alikuwa mstari wa mbele kuwaongoza wanachama wenzake wa CHAKIMO kuzuru shule mbalimbali za eneo la Eldoret kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Baada ya kuhitimu chuoni mwishoni mwa 2011, Nganga alianza kufundisha Kiswahili, Kiingereza na somo la Biashara katika Shule ya Upili ya Pumwani Girls, Nairobi. Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa zaidi kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

Ilikuwa hadi Oktoba 2012 ambapo Nganga alijiunga na kampuni ya uchapishaji vitabu ya Vide Muwa Publishers, Nairobi, akiwa Mhariri wa Kiswahili na Kiingereza.

Mnamo 2016, alipanda ngazi na kuwa Mhariri Mkuu katika kampuni hiyo. Alihudumu huko hadi Januari 2019. Baadaye alijiunga na matibaa ya One Planet Publishing & Media Services Ltd kuwa Mhariri wa Kiswahili na Kiingereza.

Uandishi

Nganga anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza rasmi tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nyingi za insha alizotunga zilimzolea sifa na kumvunia umaarufu miongoni mwa mwenzake katika shule za msingi, sekondari na hata chuoni.

Ufundi mkubwa katika michezo ya kuigiza na hadithi fupi alizozisuka ni upekee uliompandisha kwenye majukwaa ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa na za kutamanika sana katika ulingo wa Kiswahili.

Mapenzi ya kutunga mashairi na kuyaghani mbele ya hadhira ni fani iliyojikuza ndani yake tangu akiwa tineja.

Amekuwa akitunga mashairi mengi kwa minajili ya tamasha za kitaifa za muziki. Kwa sasa anapiga msasa miswada miwili ya ‘The Foresaken Tailor’ na ‘Jishinde Ushinde’ – vitabu ambavyo anaamini vitabadilisha pakubwa sura ya kufundishwa kwa masomo ya Fasihi miongoni mwa walimu na wanafunzi wengi katika shule za upili za humu nchini. Kazi hizi zitafyatuliwa hivi karibuni na kampuni ya Gateway Publishers, Kisumu.

Nganga anashikilia kwamba aliyemshajiisha zaidi kujitosa katika ulingo wa uandishi ni msomi na mwandishi maarufu wa Kiswahili Profesa Kyallo Wadi Wamitila ambaye aliihariri hadithi yake ya ‘Macho’ katika diwani ya ‘Kosa la Nani? na Hadithi Nyingine’.

Nganga anajivunia pia kuchapishiwa hadithi ‘Harubu ya Maisha’ katika mkusanyiko wa ‘Mapambazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine’.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa wa Kiswahili na mhadhiri wa chuo kikuu, Nganga anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Miongoni mwao ni Geoffrey Mwangi (Mwalimu wa Kiswahili), Elizabeth Wanjiku (Equity Bank, Murang’a), Julius Musyoka (Afisa wa Uhusiano Mwema, Shule ya Upili ya Covenant Treasures) na David Mwangi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kompyuta na teknolojia.

Nganga anatambua upekee wa mchango wa mkewe Bi Dorcas Kamanthe katika kumhimiza pakubwa kukichapukia Kiswahili.

Kwa pamoja, wamejaliwa watoto wawili: Emmanuel Mumo na Mercy Mwende ambaye kwa sasa ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Mary Mount Academy, Daystar, Athi River.