AKILIMALI: Mhandisi aliyedhihirisha unaweza kuwika afisini na pia kule shambani
Na MARY WANGARI
NANI alisema huwezi kujaaliwa yote?
James Macharia, 47, ni mhandisi na mkulima anayekosoa msemo huu na kuthibitisha fika kwamba kupitia subira, ustahimilivu na kutia juhudi, unaweza kupata yote.
Macharia ana mke na watoto watatu.
Mkulima huyu pia ameajiriwa na Taasisi ya Kimataifa kuhusu Utafiti wa Mifugo (ILRI), kama mhandisi wa Mitambo (Mechanical and Refrigeration Systems).
“Lengo langu daima limekuwa kutagusana na wanasayansi huku wakifanya tafiti kuhusu kilimo na ufugaji nami nikidhibiti mitambo na mashine zao,” anasema Macharia.
Kwa sasa anamiliki ekari 10 za ardhi na pia amekodisha ekari zingine nane za ardhi katika maeneo ya Nyeri, Nyandarua, Tharaka Nithi na Kirinyaga ambamo anaendeleza kila aina ya kilimo ikiwemo ukulima wa majanichai na kahawa, kilimo cha mboga mathalan nyanya, kabeji, spinachi, sukumawiki, viazi vyeupe, viazi vitamu, French Beans, kilimo cha nafaka; mahindi, maharage, mtama, kilimo cha matunda kama vile tikiti maji, parachichi, karakara, Macadamia na Beetroots.
“Tangu zamani, nilikuwa navutiwa na kilimo. Nililelewa na marehemu mamangu aliyekuwa ameajiriwa katika kiwanda cha kahawa mjini Nyeri. Alikuwa akinipa motisha kwamba lau taifa hili lingelikuwa na watu wanaolenga mbele tungelikuwa na viwanda vikubwa kama vile Nestle Foods kupitia uongezaji thamani,” akasema.
Msingi wa hoja yake ulikuwa kwamba ikiwa waliweza kutengeneza bidhaa za kahawa enzi za 1960, je, vipi baada ya maendeleo ya teknolojia, uzalishaji kawi, nishati safi inayofaa, soko na barabara miongoni mwa mengine?
“Mbona tumekwama katika mbinu ile ile kikazi? Hatuwezi kuongeza thamani?” anashangaa Macharia ambaye amekuwa akifanya kilimo kwa miaka minane sasa.
Licha ya ardhi yao kuwa ndogo, hakufa moyo.
Alipania kutia juhudi katika elimu na kisha hatimaye kununua ardhi na kufanyisha kazi mafunzo aliyopata kutoka kwa mamake mpendwa. Bidii yake ya mchwa ilifua dafu alipojaaliwa kipande chake cha ardhi eneo la Kinale, Nyandarua mnamo 2006.
“Sikuweza kufanya mengi kwa sababu ya vikwazo vingi vilivyotokana na masuala ya urithi. Eneo hilo pia lilikuwa na baridi nyingi na ikawa changamoto kuishi huko,” anasema.
Baadaye alinunua kipande cha ardhi kilichokuwa na takriban miti 7,500 ya majanichai eneo la Chogoria.
Apiga hatua
Kisha aliongeza vipande vingine viwili vya ardhi kutokana na mapato ya majanichai.
Anajihusisha pia na uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti katika vijisehemu vya ardhi yake ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Hakomei hapo maadamu kwenye miti hiyo ameweka mizinga ya nyuki ambapo huvuna asali!
“Kutokana na haja ya mbolea ambayo nilikuwa nikinunua, nilikata shauri 2015 kufuga ng’ombe ambao wangenipa maziwa huku nikipata mbolea. Hapo ndipo nilipokumbana ana kwa ana na changamoto za ufugaji.”
Ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ulizua haja nyingine iliyomfungulia ukurasa mwingine mpya wa mawazo.
“Niligundua ni kosa kubwa kufuga mifugo bila mikakati thabiti kuhusu jinsi ya kupata malisho yao. Ndipo nilipokodisha kipande cha ardhi eneo la Mwea kaunti ya Kirinyaga na kuanza kupanda nyasi, mahindi, mtama na hivi karibuni nyasi ya branchiaria,”
“Mke wangu aliungana nami hivi majuzi katika shughuli ya kilimo na anasimamia mashamba ya eneo la Mwea ambapo tunafanya kilimo cha matunda na mboga huku tukiendelea na malisho ya mifugo,” anasema akifichua kwamba alipata mtaji wa kuanza kilimo kutokana na akiba aliyoweka alipokuwa akifanya kazi kama mhandisi katika mashirika anuai mathalan GPL, Magnate Ventures and Agridutt.